1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi moja, chaguzi mbili

Mohammed Khelef15 Oktoba 2015

Jumapili ya 25 Oktoba, Watanzania wataelekea vituoni kuwachagua viongozi kwa miaka mitano ijayo na DW inakujuza baadhi ya yaliyo muhimu kuyajuwa juu ya uchaguzi huo na historia ya chaguzi nchini humo.

Wagombea wawili wanaochuana vikali kwenye uchaguzi huu: Edward Lowassa wa UKAWA (kushoto) na John Magufuli wa CCM.
Wagombea wawili wanaochuana vikali kwenye uchaguzi huu: Edward Lowassa wa UKAWA (kushoto) na John Magufuli wa CCM.Picha: picture-alliance/AP Photo/Getty Images/AFP/DW Montage

Mifumo mitatu ya vyama

Tanzania imepitia mifumo mitatu ya vyama vya siasa katika historia yake hadi sasa. Kabla na hata kipindi kifupi baada ya uhuru wa iliyokuwa Tanganyika hapo mwaka 1961 na Mapinduzi ya Januari 1964 visiwani Zanzibar, pande hizo mbili ambazo zilikuja kuungana baadaye kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilikuwa na mifumo ya vyama vingi vya kisiasa vilivyoshiriki kupigania uhuru kutoka kwa Muingereza.

Mwezi Aprili 1964, baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwa taifa moja, vyama viwili tafauti viliongoza kila kimoja upande wake. Tanganyika African National Union (TANU) iliendelea kutawala upande wa Tanganyika ambayo baadaye iliitwa Tanzania Bara na Afro-Shirazi Party (ASP) iliendelea kutawala upande wa Zanzibar. Kwa hivyo, nchi moja ilikuwa na vyama viwili tafauti.

Mwezi Februari 1977, TANU na ASP ziliungana na kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na hivyo kuifanya Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania kuwa chini ya chama kimoja, hali iliyoendelea hadi mwaka 1992. Chini ya mifumo ya chama kimoja na vyama viwili, chaguzi zilifanyika mwaka 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na 1990.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliiongoza CCM na Tanzania hadi mwaka 1985.Picha: Getty Images/AFP

Nchi moja, chaguzi mbili

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayoongozwa na serikali mbili ndani ya moja na hivyo chaguzi zake pia zinafanyika kwa kuakisi uhalisia huo. Kwa upande mmoja, Watanzania wa pande zote mbili (Bara na Zanzibar) watawachagua viongozi wao kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani rais na wabunge, na kwa upande mwengine Watanzania wa Zanzibar peke yao watachaguwa pia rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Vile vile, uchaguzi huu unakwenda sambamba na kuwachagua madiwani kwa pande zote mbili za Muungano. Hivyo, mpigakura wa Muungano, ataingia kwenye chumba akiwa na karatasi tatu za kura: urais, ubunge, na udiwani; huku yule wa Zanzibar akiwa na karatasi tano: rais wa Muungano, rais wa Zanzibar, mbunge, mwakilishi na diwani.

Uchaguzi wa tano wa vyama vingi

Uchaguzi huu wa mwaka 2015 ni wa tano tangu chaguzi za vyama vingi kuanza tena nchini Tanzania, ukitanguliwa na chaguzi kama hizo za mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010. Katika chaguzi zote za awali, CCM ilitangazwa kuongoza kwenye nafasi zote ilizowania katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Benjamin Mkapa alishinda urais wa Muungano mwaka 1995 kwa asilimia 61.8, akashinda tena kwa asilimia 71.7 mwaka 2000, ambapo Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80.28 mwaka 2005 na tena kwa asilimia 62.8 mwaka 2010. Kwa upande wa Zanzibar, Salmin Amour Juma alitangazwa mshindi kwa asilimia 50.2 mwaka 1995, huku Amani Abeid Karume akitangazwa kwa asilimia 67.04 mwaka 2000 na asilimia 53.1 mwaka 2005 na mwaka 2010, Ali Mohamed Shein akatangazwa mshindi kwa asilimia 50.1.

Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka huu unatazamiwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi kwa upande wa urais wa Jamhuri ya Muungano kuliko ilivyowahi kutokea kwenye chaguzi nne zilizopita. Vyama vinne vya upinzani vilivyojiunga chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vimemsimamisha aliyekuwa waziri mkuu na kada wa zamani wa CCM, Edward Lowassa kwa tiketi ya CHADEMA, huku CCM ikimuweka waziri wa ujenzi, John Pombe Magufuli.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na mgombea urais kwa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.Picha: DW

Kwa upande wa urais wa Zanzibar, Dk. Shein wa CCM anatetea nafasi yake dhidi ya Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF.

Wagombea urais wasiovuma

Mbali na Magufuli wa CCM na Lowassa wa CHADEMA/UKAWA kwa urais wa Muungano na Dk. Shein wa CCM na Maalim Seif wa CUF kwa urais wa Zanzibar, kuna wagombea sita wa vyama vingine vidogo vidogo kwa upande wa Muungano na 12 kwa Zanzibar.

Kwa urais wa Muungano, wagombea hao ni Anna Mghirwa wa ACT-Wazalendo, Fahmi Nassor Dovutwa wa UPDP, Macmillan Lyimo wa TLP, Hashim Rungwe wa CHAUMA, Janken Kasambala wa NRA, na Chifu Yemba wa ACT.

Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghirwa.Picha: ACT/Wazalendo

Miongoni mwa wagombea urais wa Zanzibar, ni Juma Khatib wa TADEA, Hamad Rashid wa ACT, Said Soud wa CCW, Seif Ali Iddi wa NRA, na Kassim Bakari Ali wa Jahazi Asilia.

Idadi ya Wapigakura na vituo vya kupigia kura

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jumla ya Watanzania milioni 22.75 wamejiandikisha kupigakura, ambapo vituo 65,105 vitatumika kupigia kura na kila kituo kikiwa na wapiga kura wasiozidi 450. Hiyo ni kwa uchaguzi wa wabunge na urais wa Muungano tu. Ndani ya idadi ya wapiga kura hao, wamo wamo pia wapigakura wa Zanzibar, ambao ni 503,193. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inahusika na uchaguzi visiwani Zanzibar pekee, huku NEC ikihusika na uchaguzi wa rais wa Muungano na ubunge kwa Tanzania nzima, na pia udiwani kwa Tanzania Bara pekee.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf