Undav aisaidia Stuttgart kuizamisha Gladbach
26 Januari 2026
Mabingwa wa kombe la shirikisho la Ujerumani Stuttgart hawakutoka jasho jingi sana dhidi ya kikosi kibovu cha Gladbach, ambao wameporomoka viwango vya soka baada ya kupoteza mechi nne kati ya sita zilizopita.
Stuttgart wako nyuma ya timu inayoshikilia nafasi ya tatu Hoffenheim, kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Hoffenheim wana mechi moja mkononi.
"Maelewano na ushirikiano wa timu umefikia kiwango kingine," alisema Denis Undav. "Tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa sana na mbinu nyingi. Haijalishi nani anayeanza na nani anayetokea mbao ndefu." Akaongezea.
Haris Tabakovic wa Gladbach alikosa penalti ya mapema kabla Jamie Leweling kufunga bao la ufunguzi.
Baada ya Joe Scally kuutia mpira katika lango lake mwenyewe, mchezaji wa akiba Undav alifunga kazi katika mechi hii kwa bao lake la dakika za lala salama.
Penalti dhaifu ya Tabakovic, iliyotolewa wakati Leweling alipounawa mpira ndani ya eneo la hatari, ilizuiwa kwa urahisi na kipa wa timu ya taifa ya Ujerumani Alexander Nuebel zikiwa zimesalia dakika 13. Ilikuwa penalti ya pili kwa Mbosnia huyo kukosa katika miezi mitatu.
Gladbach waliinamisha vichwa vyao chini na Stuttgart wakacharuka, Leweling akicheza kupitia eneo la penalti kabla ya kuutia mpira kambani baada ya nusu saa ya mchezo.
"Sikuwa kwenye mchezo wangu leo lakini kama mshambuliaji una fursa ya kufanya mambo kuwa mazuri kwa kufunga bao," Leweling aliiambia DAZN.
Kuingizwa uwanjani Undav dakika ya 61 kulikuwa ufunguo muhimu kwani mpira uliruka kutoka mgongoni mwa Scally huku akijaribu kumzuia na kumbana mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani kwenye kona.
Kisha Undav akaongeza bao lake mwenyewe zikiwa zimesalia dakika 23, akivurumisha shuti la chini kwenye kona ya chini ya lango.