1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNESCO yapata mkuu mpya

14 Oktoba 2017

Mfaransa Audrey Azoulay achaguliwa kuliongoza shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Elimu Sayansi na utamaduni UNESCO

Frankreich Audrey Azoulay soll neue Unesco-Chefin werden
Picha: picture-alliance/dpa/Chen Yichen

Bodi kuu ya uongozi ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na elimu Sayansi na Utamaduni Unesco imemchagua aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Ufaransa kuwa mkuu wa shirika hilo  baada ya kujitokeza mivutano isiyo  ya kawaida katika mchakato wa kumtafuta mkuu mpya,ambao uligubikwa zaidi na mvutano kuhusu Mashariki ya kati.

Kuchaguliwa kwa Audrey Azoulay badala ya mgombea kutoka Qatar kumekuja siku moja baada ya Marekani kutangaza nia yake ya kujiondowa katika shirika hilo kutokana na kile ilichodai kwamba linaonesha upendeleo dhidi ya Israel.Taarifa hiyo iliugubikwa mchakato mzima wa uchaguzi katika kipindi cha wiki moja ambao tangu hapo ulikuwa umeshakumbwa na mihemko na mashaka ya mivutano ya siasa za kikanda  kukiwepo wasiwasi kuhusu suala la ufadhili wa shirika hilo lenye makao makuu yake Ufaransa ambao hauko katika hali nzuri huku pia yakiwepo maswali juu ya mwelekeo wake wa baadae.

Mgombea wa Qatar aliyeshindwa-Hamad bin Abdel Aziz al-KawariPicha: Getty Images/AFP/K. Sahib

Ikiwa baraza kuu ya UNESCO litamuidhinisha Azoulay katika mkutano wake mkuu mwezi ujao basi atachukua nafasi ya mkurugenzi mkuu wa sasa Irina Bokova kutoka Bulgaria ambaye muhula wake wa miaka minane ulikumbwa na mivutano ya kifedha pamoja na kukosolewa juu ya kuijumuisha Palestina mwaka 2011 kuwa mwanachama wa shirika hilo.Azoulay alimshinda kwa kura chache  mgombea wa QatarHamad bin Abdulaziz al-Kawari ambapo matokeo ya mwisho yalimpa ushindi mfaransa huyo wa kura 30 dhidi ya 28.

Ushindi wake huo umekuja baada ya kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi baada a kusmhindi mshindi wa tatu kutoka Misri siku ya Ijumaa asubuhi.Matokeo ya ushindi huo wa Azoulay ni pigo kubwa kwa nchi za kiarabu ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikitaka kupata nafasi ya kuliongoza shirika hilo la Umoja wa Mataifa. Shirika hilo limewahi kuongozwa na raia wa Ulaya,Asia,Afrika na Marekani lakini halijawahi kuwa na kiongozi kutoka nchi za kiarabu.Baada ya kushinda nafasi hiyo Azoulay mwenye umri wa miaka 45 alisema hatua ya kukabiliana na matatizo ndani ya UNESCO zinapaswa kuwa ni mageuzi ya shirika hilo na wala sio kulikimbia.

Mgombea wa Misri Muschira ChattabPicha: picture alliance/dpa/AA/M. Elshemy

Mkurugenzi mkuu huyo mpya ataweka vipaumbele vya shirika hilo linalofahamika kwa mpango wake wa turathi za dunia katika kulinda maeneo ya kitamaduni na utamaduni.Kadhalika shirika hilo hufanya kazi ya kuimarisha eleimu kwa ajili ya watoto wa kike pamoja na kuutanabahisha ulimwengu kuhusu ukatili na mauaji ya kutisha yaliyofanyika dhidi ya wayahudi(Holocoust),linatetea pia uhuru wa vyombo vya habri na kuratibu shughuli za kisayansi na mabadiliko ya tabia nchi.Kadhalika mkuu mpya atalazimika kukubalina na hali ya kujiondowa kwa Marekani na Israel ambayo imeunga mkono hatua ya mshirika wake kwa kuitetea na kusema kwamba nayo itajiondoa katika shirika hilo.Hata uchaguzi wenyewe uligeuka kuwa mchakato wa kisiasa hata kabla ya Marekani kutangaza kujiondoa .

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:John Juma