1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNESCO yasema watoto milioni 250 duniani hawajui kusoma na kuandika

Mjahida30 Januari 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na tamaduni UNESCO limesema watoto milioni 250 wa shule ya msingi duniani kati ya watoto milioni 650 hawajui kusoma na kuandika na hata kufanya hesabu rahisi.

Wanafunzi darasani barani Afrika
Wanafunzi darasani barani AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Ripoti hiyo imegundua watoto milioni 130 wako katika shule za msingi lakini bado hawajapata kiwango kinachohitajika cha mafunzo huku milioni 120 ya watoto hao, wakiripotiwa kuwepo muda mchache madarasani na wengine wakiripotiwa kutoingia madarasani kabisa, wakiwemo Milioni 57 ya vijana wadogo wasiokwenda shule.

Kundi linalojitegemea lililoandika ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na tamaduni UNESCO, limekadiria kuwa kwa watoto milioni 250 kutokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika katika maeneo mengi duniani, kunatoa hasara ya takriban dola bilioni 129 kila mwaka kwa serikali.

Muakilishi wa UNESCO Vibeke Jensen amesema hali hii aliyoiita janga la masomo inasababishwa na kutokuwa na walimu walio na ujuzi wa kutosha.

Nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na tamaduni UNESCO

Akizungumza na waandishi habari wakati wa kuzindua ripoti hiyo Vibeke amesema kitu kinachohitajika kwa sasa ni kuwepo njia za kuboresha elimu kwa wanafunzi kote duniani.

Walimu zaidi kusajiliwa kabla ya mwaka 2015

Ripoti hiyo pia imesema chini ya asilimia 75 ya walimu wamepewa mafunzo ya kukidhi mahitaji ya elimu kitaifa. Katika taarifa ya Rina Bokova Mkurugenzi mkuu wa UNESCO, walimu ndio waliobeba maisha ya kizazi hiki katika mikono yao, na kutokana na hilo takriban walimu milioni 5.2 wanahitaji kusajiliwa ifikapo mwaka wa 2015 huku akisisitiza walimu hao waungwe mkono katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Hata hivyo kundi lililofanya utafiti kwa shirika la UNESCO limesema nusu ya milioni 57 ya watoto ambao hawaendi shule wako katika maeneo yaliokumbwa na migogoro.

Idadi hiyo inasemekana kuongezeaka kutoka asilimia 42 mwaka wa 2008. Inakadiriwa kuwa nchi 14 zina watoto zaidi ya milioni moja walioacha shule mwaka wa 2011 ikiwemo Afghanistan, China, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia, Sudan kabla ya kugawika pamoja na Tanzania.

Wanafunzi darasaniPicha: UNESCO/E. Jansson

Lakini licha ya hayo nchi tatu zimeripotiwa kupunguza kwa asilimia 85 idadi ya wanafunzi wanaoacha shule katika kipindi cha miaka mitano iliopita. nchi hizi ni Laos, Rwanda, na Vietnam. Viongozi wa dunia waliweka malengo mwaka wa 2000 ya kutoa elimu kwa kila mtoto katika shule ya msingi ifikapo mwaka wa 2015, lakini kulingana na ripoti hii ya UNESCO malengo hayo yanaonekana kutotimizwa kwa kiwango kikubwa.

Eneo la jangwa la Afrika ndilo lililonyuma kabisa katika kutoa elimu kwa wanafunzi wa eneo hilo. Watafiti wanasema iwapo hali hiyo itazidi kuendelea vijana waliomatajiri watafanikiwa kumaliza masomo yao ya msingi mwaka wa 2021 huku vijana wa kike walio masikini wakibaki nyuma na kukadiriwa kumaliza masomo yao ya msingi mwaka wa 2086.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman