1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR: Watu milioni 70.8 wanaishi kama wakimbizi duniani

Daniel Gakuba
19 Juni 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi, UNHCR limesema watu takriban milioni 71 wameyakimbia makazi yao duniani kote, kuepuka ghasia na unyanyasaji. Miongoni mwao milioni 41 ni wakimbizi wa ndani ya nchi zao.

Kolumbien Flüchtlinge
Picha: Getty Images/G. Legaria

Ripoti hiyo ya UNHCR imetangazwa kwenye mkesha wa siku ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi ambayo inaadhimishwa kesho Alhamis. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu milioni 70.8 walilazimika kuyahama makazi yao mwaka uliopita, hilo likiwa ongezeko la watu karibu milioni mbili ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Miongoni mwa hao, zaidi ya milioni 41 ni wakimbizi wa ndani ya nchi zao.

Akiizindua ripoti hiyo mapema leo mjini Geneva, Kamishna wa UNHCR  Filippo Grandi amesema kwa bahati mbaya hali inachukua mwelekeo usio sahihi, na kwamba imeibuka mizozo mpya ambayo inaongeza idadi ya wakimbizi juu ya waliokuwepo ambao tayari ni wengi. Grandiamepinga dhana kwamba wote wanaozihama nchi zao ni wakimbizi wa kimaslahi.

Filippo Grandi: Kamishna wa Shirika la UNHCRPicha: Reuters/D. Balibouse

''Watu huyahama makazi yao kwa sababu mbalimbali, ambazo tunaweza kuziita za mseto. Bila shaka, wapo wanaoondoka kutafuta fursa bora za kiuchumi, lakini, na wapo wengine ambao wanakimbia ghasia na vitisho vikubwa wanavyofanyiwa.'' Amesema Grandi.

Idadi yaongezeka sambamba na muda

Kiongozi huyo wa UNHCR amesema matatizo ya wakimbizi yanaongezeka kwa idadi yao na kwa muda wanaoishi uhamishoni. Amesema asilimia 80 wamekuwa wakimbizi kwa zaidi ya miaka 5.

Wakimbizi waliovikimbia vita vya Syria vilivyodumu sasa kwa miaka minane, ndilo kundi kubwa, wakifika karibu milioni 13. Kundi jingine la wakimbizi wengi kutoka nchi moja ni la Wavenezuela, ambao ni zaidi ya 340,000.

Marekani inaendelea kuongoza katika michango ya kuwafadhili wakimbiziPicha: DW/E. van Nes

Ripoti hiyo kuhusu wakimbizi inaonyesha kuwa watu milioni 4 wamezihama nchi za Amerika Kusini mnamo miaka ya hivi karibuni, lakini ni mmoja tu kati ya wanane ambaye ambaye ameomba rasmi hifadhi ya ukimbizi, ikimaanisha kuwa wengine wanabakia kuwa mzigo kwa jamii walikokimbilia.

Marekani bado ndio mchangiaji mkubwa wa fedha

Filippo Grandi amesema Marekani bado ndio mfadhili mkubwa wa shughuli za kuwasaidia wakimbizi ulimwenguni, lakini amekosoa kauli kali dhidi ya wakimbizi ambazo zimejitokeza hivi karibuni, sio Marekani tu bali Ulaya pia ambapo wakimbizi na wahamiaji wanachukuliwa kama watu waliokuja kuwapokonya wenyeji fursa zao za ajira, na kutishia usalama na maadili yao ya kijamii.

Katika ripoti ya leo UNHCR imesisitiza kwamba idadi kubwa kabisi ya wakimbizi na wahamiaji iko katika nchi zanazoendelea, sio katika mataifa tajiri. Imeonyesha pia kwa miaka saba mfululizo, idadi ya wakimbizi imekuwa ikipanda, kila mwaka ukivunja rekodi ya uliotangulia.

ape,afpe