UNHCR: Watu wanaoomba hifadhi waongezeka
26 Machi 2015Takwimu hizo mpya ziko katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi-UNHCR, iliyozinduliwa leo, ambapo kwa mwaka uliopita wa 2014, watu 866,000 waliomba hifadhi kwenye mataifa ya Magharibi, ikiwa ni kiwango cha juu kwa miaka 22.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mataifa 44 tajiri duniani, yalipokea maombi hayo ya hifadhi mwaka uliopita, huku Ujerumani ikiwa nchi inayoongoza kwa kuwa na maombi 173,000. Nusu ya maombi hayo yametoka kwa wakimbizi wa Syria. Marekani imeshika nafasi ya pili ambapo imepokea maombi 120,000 ya watu wanaotaka hifadhi.
Msemaji wa shirika la UNHCR, Melissa Fleming amewaambia waandishi wa habari kuwa hali hiyo imesababisha mzozo mbaya wa kibinaadamu. Amesema idadi hiyo ni kubwa tangu mwaka 1992 ambapo watu 900,000 waliomba hifadhi kwenye mataifa tajiri kutokana na vita vya Bosnia na Herzegovina.
Ripoti hiyo imesema Ujerumani na Marekani zimefuatiwa na Uturuki, Sweden na Italia. Mkuu wa UNHCR, Antonio Gutteres, amesema mizozo inayoendelea sehemu mbalimbali duniani inalipa shirika hilo changamoto kubwa. Amesema wanajitahidi kuhakikisha watu wanaokimbia vita wanapata hifadhi, fursa ya kuwa na makaazi na huduma nyingine muhimu za kuwalinda.
Wakimbizi milioni 3.9 hawako kwenye takwimu za ripoti mpya
Hata hivyo, UNHCR imesema takwimu hizo ni za chini ikilinganishwa na wakimbizi walioko Lebanon, Jordan na Uturuki. Ripoti hiyo imeeleza kuwa kiasi wakimbizi milioni 3.9 waliopelekwa kwenye nchi hizo, hawako kwenye takwimu za sasa za ripoti hiyo iliyopewa jina ''Mwenendo wa Watu wanaoomba Hifadhi mwaka 2014.''
Flemming amesema mwaka 2013, watu 596,000 ndiyo waliomba hifadhi kwenye mataifa tajiri. Wasyria 150,000 waliomba hifadhi mwaka uliopita, huku Iraq ikishika nafasi ya pili baada ya watu wake 68,000 pia kuomba hifadhi.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, Uturuki ilikuwa na zaidi ya wakimbizi milioni moja na nusu wa Syria, huku ikipokea maombi 87,800 ya watu wanaotaka hifadhi, wengi wao wakiwa ni kutoka Iraq. Watu hao waliyakimbia makaazi yao, baada ya kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, kuyadhibiti maeneo kadhaa ya nchi hiyo.
Sweden ambayo imeshika nafasi ya nne kulingana na ripoti hiyo, kwa upande wake imepokea maombi 75,100, hasa kutoka Syria na Eritrea. Flemming amesema Wairaq wengi wanakimbilia Uturuki, huku Ujerumani na Sweden zikiwachukua Wasyria wanaoomba hifadhi kwenye nchi hizo. Wakati huo huo, ripoti hiyo imesema raia 15,700 wa Ukraine wameomba hifadhi katika mataifa 44 yaliyoendelea kiviwanda duniani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel