1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR yafunga shughuli katika kituo cha wakimbizi Tripoli

31 Januari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi - UNHCR limesema linasitisha operesheni zake katika kituo cha muda cha wakimbizi mjini Tripoli, Libya kutokana na hofu ya kulengwa katika mashambulizi ya kijeshi

Libyen Migranten im Lager nahe Tripoli
Picha: Getty Images/AFP

UNHCR imesema inafahamu kuwa mazoezi ya kijeshi na polisi yanafanyika umbali wa mita kadhaa kutoka kituo hicho, ambacho kinawahifadhi waomba hifadhi na wakimbizi. Mkuu wa ujumbe wa UNHCR nchini Libya Jean-Paul Cavalieri amesema wameanza kuwahamishia maeneo salama wakimbizi walio katika hatari kubwa, na ambao wanasubiri kupewa makazi mapya. Ameongeza kuwa watawahamisha mamia ya wengine na kuwapeleka katika maeneo ya mijini.

Kituo hicho kilianzishwa kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi wanaosubiri kuhamishiwa ng'ambo. Mamia ya watu wanaoishi kituoni hapo walichukuliwa mwaka jana baada ya kukimbia vituo vingine ambavyo viliathirika na mapigano.

Julai mwaka jana, watu 53 waliuawa na 130 wakajeruhiwa katika mashambulizi ya angani kwenye kituo kimoja cha wahamiaji na wakimbizi kwenye kitongoji kimoja cha Tripoli, wakati kukiwa na mapigano kati ya serikali ya umoja wa kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli na vikosi vya Libyan National Army vikiongozwa na Kamanda Khalifa Haftar. Serikali ya Tripoli ilivilaumu vikosi vya Haftar, ambavyo vilikanusha kukilenga kituo hicho.

Pande zote za mgogoro wa Libya zinalaumiana kwa kuvunja mpango wa kusitisha mapiganoPicha: picture-alliance/Photoshot/H. Turkia

Mjumbe wa Umoja wa MataIfa nchini Libya, Ghassan Salame amezituhumu nchi za kigeni kwa kuendelea kuingilia mzozo wa Libya, kinyume na ahadi zilizotolewa katika mkutano wa kilele wa kimataifa mjini Berlin mwezi huu. Amesema pande za ndani nan je ya Libya zinaonekana kuunga mkono juhudi za kuhimiza amani lakii zinaendelea kutaka suluhisho la kijeshi.

Ghassane ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia mawasiliano ya video kutokea Brazzaville kuwa mbinu za kisiri za kuzipa silaha pande zinazozozana licha ya kuwepo marufuku ya Umoja wa Mataifa zinatishia kuanzisha machafuko mapya na ya hatari Zaidi. 

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika umesema kuwa Algeria imependekeza kuandaa kongamano la maridhiano kuhusu Libya wakati wa mkutano wa viongozi wa Afrika unaojadili mbinu za kumaliza mzozo huo.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame, pamoja na marais kadhaa wa Afrika.

Viongozi hao wa Afrika walitarajiwa kukutana katika kikao cha faragha na mkuu wa serikali ya Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa Fayez al-Sarraj, na baadaye na wajumbe kutoka upande wa Kamanda Khalifa Haftar, anayedhibiti mashariki mwa Libya. Viongozi hao wa Afrika ni pamoja na marais wa Congo-Brazzaville, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya jana, pamoja na wa Mauritania na Djiubouti. Hakukuwa na tangazo rasmi kama mikutano huyo ilifanyika.