1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR yahofia Waafghanistan zaidi wataikimbia nchi yao

Zainab Aziz Mhariri:Rashid Chilumba
13 Julai 2021

Kuna uwezekano kwamba raia wengi zaidi wa Afghanistan wakakimbia makazi yao kutokana na ghasia zinazozidi kuongezeka. Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR limetoa taarifa hiyo. 

Afghanistan | Familien fliehen aus der Provinz Kandahar
Picha: Mohammad Ibrahim/DW

Shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetoa tahadhari hiyo wakati ambapo kundi laTaliban linaendelea kuyadhibiti maeneo zaidi nchini Afghanistan tangu kuondoka kwa vikosi vya kigeni vilivyokuwa vinaongozwa na Marekani.

Msemaji wa Kamishna wa Wakimbizi wa shirika la UNHCR Babar Baloch, amesema kwenye mkutano mjini Geneva kwamba Afghanistan iko ukingoni kutumbukia kwenye mgogoro mwingine wa kibinadamu na kwamba hali hii inaweza kuepukwa na inapaswa kuepukwa. Baloch amesema juhudi za kuwezesha kupatikana amani zinapaswa kuimarishwa kwani hilo ndilo wanalolitarajia raia wa Afghanistan.

Familia zikijiandaa kuondoka kutoka kwenye eneo la Kadhahar wanakimbia vuruguPicha: Mohammad Ibrahim/DW

Baloch amesema takriban Waafghanistan 270,000 tayari wameyakimbia makazi na hivyo wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani tangu mwezi Januari, na kulingana na idadi hiyo inamaanisha kuwa hadi sasa zaidi ya watu milioni 3.5 wamelazimika kuondoka na kuyaacha makazi yao nchini Afghanistan. 

Msemaji wa Kamishna wa Wakimbizi wa shirika la UNHCR Babar Baloch ameeleza kuwa wakimbizi hao wanalalamika juu ya hali mbaya ya usalama, unyang'anyi unaofanywa na makundi ya wahalifukuzagaa na vifaa vya kulipuka kwenye barabara nyingi kuu na pia watu kupoteza njia za kuwaletea mapato na ukosefu wa huduma za kijamii.

Rais wa Marekani Joe Biden amekiri kwamba kwa Afghanistan bado iko mbali mno hadi itakapofikia hali ya utulivu lakini amesema watu wa Afghanistan ndio wenye jukumu la kuamua hatima yao.

Kushoto: Jenerali Scott Miller aliyeongoza vikosi vya Marekani nchini AfghanistanPicha: Ahmad Seir/AP/picture alliance

Jenerali wa Marekani aliyeongoza vita nchini Afghanistan, Scott Miller siku ya Jumatatu aliaga rasmi katika sherehe zilizofanyika kwenye mji mkuu, Kabul na kisha aliondoka kutoka nchini humo kimya kimya hiyo ikiwa ni ishara ya mwisho ya mgogoro mrefu zaidi kuwahi mkusimamiwa na Marekani.

Wakati huo huo kiongozi mwandamizi wa kundi la Taliban amesema wao hawataki kupigana na vikosi vya serikali ndani ya miji ya Afghanistan na badala yake amewataka wanajeshi wa serikali wijisalimishe, na pia ameionya Uturuki dhidi ya kuongeza vikosi vyake nchini Afghanistan.

Vyanzo:/RTRE/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW