1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR yakataa kufanyika kwa mjadala wa Xinjiang

7 Oktoba 2022

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limepiga kura dhidi ya kufanyika kwa mjadala kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki katika eneo la Xinjiang, China hatua ambayo ni kikwazo kikubwa kwa mataifa ya Magharibi.

Großbritannien London | Protest gegen Menschenrechtsverletzungen in China
Picha: Alexander Mak/NurPhoto/picture alliance

Marekani na washirika wake mwezi uliopita waliwasilisha rasimu ya uamuzi wa kwanza kwa chombo cha juu cha haki katika Umoja wa Mataifa wakiilenga China, wakitaka angalau kufanya majadiliano kuhusu Xinjiang.  

Hatua hiyo inajiri baada ya mkuu wa zamani wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet kutoa ripoti yake kuhusu Xinjiang aliyoicheleweshwa kwa muda mrefu mwezi uliopita, akitaja uwezekano wa kufanyika uhalifu dhidi ya binadamu miongoni mwa jamii ya Uyghur na Waislamu wengine walio wachache katika eneo hilo la magharibi.

soma UN: China huenda ilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Xinjiang

Lakini kufuatia ushawishi mkubwa wa Beijing, nchi za baraza la wanachama 47 huko Geneva zilipiga kura 19 dhidi 17 ya kupinga mjadala, huku nchi 11 zikijizuia kushiriki katika kura hiyo.

Mataifa yaliyopiga kura ya kupinga kufanyika kwa mjadala huo yalikuwa Bolivia, Cameroon, China, Cuba, Eritrea, Gabon, Indonesia, Ivory Coast, Kazakhstan, Mauritania, Namibia, Nepal, Pakistan, Qatar, Senegal, Sudan, Falme za Kiarabu, Uzbekistan na Venezuela.

Waliojizuia ni Argentina, Armenia, Benin, Brazil, Gambia, India, Libya, Malawi, Malaysia, Mexico na Ukraine.

 Ubaguzi wa kimfumo

Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Balozi wa Uingereza Simon Manley aliomba rai ya kuungwa mkono kwa mjadala huo akisema "Sisi ni wajumbe wa Baraza la Haki za Kibinadamu. Tuko hapa kuinua hali ya ubaguzi wa kimfumo. Tuko hapa kujadili ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu na ukiukwaji punaofanywa popote na kwa yeyote."

"Hakuwezi kuwa na shaka juu ya uzito na ukubwa wa kile kinachoripotiwa katika Xinjiang uthibitisho wa mjadala kama huo. Hivyo basi, nitoe rai kwa wajumbe wenzetu wa baraza hili kufanya kilicho sahihi, tusifumbie macho, bali tuunge mkono uamuzi huo, ili tu kufanya mjadala. Hakuna zaidi, hata kidogo."

Uamuzi wa rasimu hiyo ulifadhiliwa na Uingereza, Kanada, Sweden, Denmark, Finland, Iceland, Norway, Australia na Lithuania. Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za Magharibi alisisitiza kwamba bila kujali matokeo,  "lengo nambari moja limetimizwa" katika kuweka uangalizi kwa Xinjiang.

Ripoti ya Bachelet, ambayo ilichapishwa Agosti 31 kabla ya muda wake kumalizika, iliangazia madai "ya kuaminika" ya kuenea kwa mateso, kuwekwa kizuizini kiholela na ukiukwaji wa haki za kidini na uzazi. 

Michelle BacheletPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Beijing ilikataa vikali madai hayo na kushutumu Umoja wa Mataifa kwa kile walichotaja kama kuwa "jambazi na mshirika wa Marekani na Magharibi". Na inasisitiza kuwa inaendesha vituo vya mafunzo ya ufundi katika kanda hiyo ili kukabiliana na itikadi kali.

"Kwa kweli ni wito mgumu kwa nchi nyingi." "Mapambano yanaendelea."  alikiri mwanadiplomasia Simon Manley.