1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 yawaingiza watoto milioni 150 kwenye umasikini

17 Septemba 2020

Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF na Shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto la Save the children umeonyesha janga la COVID-19 limewatumbukiza watoto milioni 150 kwenye umasikini.

Brasilien, Kinderarmut
Picha: Getty Images/R.Alves

Kwa mujibu wa mashirika hayo ya kuwahudumia watoto, tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona, kumekuwa na ongezeko la asilimia 15 la idadi ya watoto wanaoishi katika mataifa masikini na yale ya kipato cha kati, na kuifikisha idadi jumla kuwa takriban bilioni 1.2.

Ripoti hiyo iliyochapishwa siku ya Alhamisi imezieleza takwimu hizo kwa kuangazia masuala kadhaa kama vile kukosekana kwa upatikanaji wa elimu, huduma za afya na makaazi. Mashirika hayo yameonya kuwa watoto masikini duniani wanazidi kuwa masikini na hali hii inaweza ikawa mbaya zaidi katika miezi ijayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema familia ambazo zilikuwa katika hatua ya kuondokana na umasikini zimerudishwa nyuma, huku nyingine zikikabiliwa na viwango vya umasikini ambao hazijawahi kuushuhudia hapo kabla. Fore amezitolea wito serikali kuongeza haraka mfumo wa ulinzi, upatikanaji wa huduma ya afya pamoja na fursa kwa watoto kupata mafunzo ya mbali kwa njia ya mtandao.

Mtoto akionyesha simu anayoitumia kwa mafunzo ya mtandaoniPicha: UNICEF/Soares

''Leo, ikiwa karibu miezi tisa tangu kuzuka kwa virusi vya corona, takwimu za UNICEF zinaonesha kuwa kiasi ya watoto milioni 463 duniani ambao shule zao zilifungwa wakati wa ugonjwa wa COVID-19, hawakuweza kupata mafunzo ya mbali kwa njia ya mtandao. Hii inatokana na ukosefu wa mtandao wa intaneti, kompyuta au simu za mkononi. Wanafunzi milioni 872 au nusu ya idadi ya wanafunzi duniani kwenye nchi 51 bado hawawezi kurejea kwenye madarasa yao,'' alifafanua Fore.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa shirika la Save the children, Inger Ashing ameonya kuwa watoto ambao wanakosa elimu wako katika hatari ya kutumbukia katika ajira za watoto au ndoa za mapema na kunaswa na mzungumko wa umasikini kwa miaka kadhaa ijayo.

Ashing amebainisha kuwa janga la virusi vya corona tayari limesababisha dharura kubwa zaidi ya elimu duniani katika historia na kwamba ongezeko la umasikini litalifanya suala hili kuwa gumu zaidi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na familia zao kukabiliana na athari zake.

Utafiti huu wa UNICEF na Save the children umehusisha takwimu kutoka katika zaidi ya nchi 70 uliojikita zaidi katika kuangalia iwapo watoto wananyimwa elimu, dawa, makaazi, chakula, usafi wa mazingira pamoja na maji.

(DPA, DW https://bit.ly/3mEHlcK)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW