1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: mamilioni ya watoto kukabiliwa njaa Yemen

26 Juni 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto, Unicef limeonya kwamba mamilioni ya watoto huenda wakatumbukia kwenye janga la njaa,huku mripuko wa virusi vya Corona ukiwa umesambaa nchini humo.

Jemen Wasserkrise
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/M. Alwafi

Kitisho hicho kinafuatia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ufadhili wa kifedha wa msaada wa kibinadamu. Onyo la Unicef linatolewa leo(Ijumaa) na limetolewa kwenye ripoti ya shirika hilo iliyoiangazia miaka mitano ya Yemen kuhusu hali ya watoto,mgogoro na janga la ugonjwa wa Covid-19. Ripoti hiyo inasema idadi ya watoto wenye utapia mlo nchini humo inaweza kufikia milioni 2.4 kufikia mwishoni mwa mwaka huu ikiwa ni idadi iliyoongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na iliyokuwepo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limekwenda mbali zaidi na kuonya kwamba wakati mfumo wa kiafya wa Yemen ulioporomoka na miundo mbinu ikiwa katika hali ya kupambana kuhimili janga la virusi vya Corona,tayari hali mbaya inayowakabili watoto huenda ikazidi kuharibika.

Limesema miundo mbinu mibovu ya huduma ya afya nchini Yemen haiko kwenye hali ya kuweza kupambana na janga la ugonjwa huu wa kusambaa kwa kasi na hasa baada ya miaka mitano ya vita kati ya wanajeshi wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na wanambambo wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Vita vinavyoendelea vimesababisha mkwamo Yemen

Kijana akiwa vitani YemenPicha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Vita hivyo ambavyo kwa kiasi kikubwa kimekwamisha sehemu kubwa ya nchi, pia vimechangia mgogoro mkubwa wa kibinadamu duniani. Mgogoro huu ulizuka mwaka 2015 wakati jeshi la muungano likiongozwa na Saudia lilipoingilia kati nchini Yemen kwa niaba ya serikali iliyotambuliwa kimataifa ambayo wanamgambo wakihouthi waliisababisha ikimbie kutoka mji mkuu Sanaa pale waasi hao walipoutwaa na kuudhibiti mji huo pamoja na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen mwaka mmoja kabla.

Shirika la Unicef linasema hali ya Yemen itaendelea tu kuwa mbaya kutokana na nchi wafadhili hivi karibuni kukata misaada yao. Kufikia sasa nchi hiyo ya kiarabu imerikodi rasmi visa 1000 vya maambukizi ya Covid-19 ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona huku idadi ya waliokufa ikifikia watu 275. Hata hivyo idadi halisi ya visa vya maambukizi inasadikika kuwa inaweza kuzidi hiyo iliyotajwa rasmi kutokana na ukosefu wa nyenzo za upimaji wa watu.

Soma zaidi: Yemen itaporomoka iwapo hakutakuwa na ufadhili zaidi

Mwakilishi wa Unicef Yemen Sara Beysolow anasema ikiwa hawatopokea msaada wa dharura wa fedha watoto watatumbukia kwenye baa la njaa na wengi watakufa na hapana shaka jumuiya ya Kimataifa itakuwa imetuma ujumbe unaoashiria kwamba maisha ya watoto hayajalishi. Mwanzoni mwa mwezi Juni ulifanyika mkutano wa kimataifa ulioongozwa na Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia ambapo nchi wafadhili 31 ziliahidi kutowa dola bilioni 1.35 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu kiwango ambacho hakikufikia kile kilichotakiwa na mashirika ya msaada.

Na katika fedha hizo Unicef ilihitaji dola milioni 461 kwa ajili ya kusimamia sehemu yake ya msaada wa kiutu lakini iliambulia kupata asilimia 10 tu ya fedha ilizohitaji. Kwa upande mwingine ilihitaji dola milioni 53 za kupambana na athari za Covid-19 kwa upande wa watoto lakini kwa mujibu wa ripoti yake shirika hilo liliambuliwa kupata asilimia 40 tu katika fungu hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW