1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Mataifa tajiri yahatarisha maisha ya watoto

24 Mei 2022

Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa limeyashutumu vikali mataifa tajiri ulimwenguni kwa kuhatarisha maisha ya watoto kote duniani kutokana na uzalishaji mkubwa wa gesi za sumu zinazoathiri afya zao.

Schweiz Genf | UNICEF Logo
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

UNICEF imesema ni wazi kuwa mataifa tajiri yanaandaa mazingira yasiyo salama kwa watoto waliomo ndani ya mataifa hayo na hata walio kwenye maeneo mengine duniani, ikiyataka mataifa hayo kupunguza viwango vya uchafu na kukata uzalishaji wa gesi zinazoliathiri tabaka hewa. 

Kituo cha Utafiti cha UNICEF kimefanya utafiti kwenye mataifa 39 ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, na Umoja wa Ulaya, kikizingatia vipengele mbalimbali, vikiwemo vya matumizi ya dawa za kuulia wadudu mashambani, kiwango cha unyevunyevu majumbani, madini ya risasi kwa watoto, kupata mwangaza na uzalishaji wa uchafu. 

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, Uhispania, Ireland na Ureno zimefanya vizuri zaidi kwenye maeneo hayo, lakini hakuna hata nchi moja iliyotafitiwa ambayo imegundulika kuwa na mazingira mazuri kwa afya za watoto. 

"Sio tu kwamba tajiri yanashindwa kuweka mazingira mazuri kwa afya za watoto ndani ya mipaka yao, bali pia yanachangia kwenye uharibifu wa mazingira ya watoto kwenye maeneo mengine ulimwenguni," alisema mkurugenzi mkuu wa kituo hicho, Gunilla Olsson.

Nchi tajiri kiuchumi zatakiwa kupunguza umasikini duniani

02:02

This browser does not support the video element.

Mataifa masikini yana mchango mdogo

Watoto ndio waathirika wakubwa wa uchafuzi wa mazingira unaofanywa na mataifa tajiri ulimwenguni.Picha: Mohammed Mohammed/Photoshot/picture alliance

Ripoti hiyo inaonesha kwamba mataifa yasiyo na utajiri mkubwa ya Amerika Kusini na Ulaya yamekuwa na athari ndogo kwenye hali ya jumla ya dunia yanapolinganishwa na mataifa tajiri zaidi yaliyofanyiwa utafiti huo.

Norway, Ireland na Finland zinatajwa na ripoti hiyo kuongoza kwenyeuwekaji wa mazingira mazuri kwa afya za watoto wao wenyewe, lakini kwenye mchango wao kwa ulimwengu ziko kwenye nafasi za chini kabisa kutokana na uzalishaji wao wa gesi chafu, kiwango cha utupaji wa takataka za kieletroniki na utumiaji. 

Katika mataifa ya Iceland, Latvia, Ureno na Uingereza, mmoja katika kila watoto watano anakumbana na jalala na uchafu mwengine nyumbani kwao, ambapo nchini Cyprus, Hungary na Uturuki, idadi hiyo ni takribani wawili kwa kila wanne.

UNICEF imegunduwa kuwa watoto wengi wanavuta hewa yenye sumu wakiwa ndani na nje ya nyumba zao, hasa nchini Mexico, ingawa hali hiyo haikutikani katika mataifa ya Finland na Japan.

Nchini Ubelgiji, Israel, Uholanzi, Poland, Jamhuri ya Czech na Uswisi, zaidi ya mtoto mmoja katika kila kumi na mbili wako kwenye hatari ya kuvuta hewa iliyoharibiwa kwa madawa ya kuulia wadudu mashambani, inasema ripoti hiyo.

Kwa ujumla, katika mataifa 39 yaliyofanyiwa utafiti huo, zaidi ya watoto milioni 20 walikutwa na kiwango cha juu cha madini ya risasi kwenye damu zao.