Unicef: Ndoa za utotoni zimepungua duniani
6 Machi 2018Ripoti hiyo ya Unicef iliyochapishwa Jumanne, inaonyesha kuwepo upungufu wa ndoa za utotoni zipatazo milioni 25 duniani tangu mwaka 2008, kutokana na kampeni ya kupinga ndoa hizo. Kulingana na ripoti hiyo, nchi za Kusini mwa Asia zilipiga hatua kubwa zaidi kivitendo.
Wanaharakati dhidi ya ndoa za utotoni na maafisa wa taasisi zinazohusika katika kampeni hiyo wanasema mafanikio yamepatikana kutokana na kuongezeka kwa elimu, pamoja na uhamasishaji wa umma kuelewa madhara yatokanayo ndoa hizo.
Pamoja na hayo lakini Unicef imeonya kwamba hadi mwaka 2030, wasichana wapatao milioni 150 wanakabiliwa na hatari ya kuozwa kabla ya kutimiza miaka 18, ikiwa juhudi zaidi hazitachukuliwa. Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo endelevu, yanaazimia kumaliza kabisa ndoa za utotoni ifikapo mwaka huo wa 2030.
Tatizo lahama kutoka India hadi Afrika
Maendeleo makubwa yamepatikana India ambako idadi ya wasichana wanaoozwa wakiwa wadogo imepungua kwa takriban asilimia 50. Mkuu wa Unicef nchini India Javier Aguilar amesema kuwa kwa sasa ni asilimia 27 ya wasichana wa India wanaoolewa kabla ya kufika umri wa utu uzima, ikilinganishwa na asilimia 47 muongo mmoja uliopita.
Ripoti ya Unicef inaonyesha kwamba matatizo ya ndoa za utotoni yamehama kutoka Ukanda wa Asia Kusini na kuelekea katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Imeelezwa kuwa mmoja kati ya wasichana wanaoolewa wakiwa watoto, anatoka katika nchi hizo za Afrika. Hii inadhihirisha kuwa nchi hizo zimebaki nyuma, kwani miaka 10 iliyopita kiwango hicho kilikuwa msichana mmoja kati ya watano.
Mfano mwema barani Afrika umetajwa kuwa Ethiopia ambayo imepunguza sana ndoa za utotoni, na kuondoka katika nchi tano zinazoongoza kwa kuwa na ndoa za aina hiyo.
Madhara ya muda mrefu
Kwa mujibu Unicef, wanawake milioni 650 duniani kote waliolewa wakiwa watoto. Makadirio ya shirika hilo ni kuwa kwa wakati huu, wasichana milioni 12 huolewa mwaka duniani kote kabla ya kutimiza miaka 18.
Mshauri mkuu kuhusu masuala ya jinsia katika shirika la Unicef Anju Malhotra amesema msichana akilazimishwa kuolewa akiwa mdogo, anakabiliwa na athari za hapo hapo na za muda mrefu. Uwezekano wake wa kupata elimu unapungua, huku hatari za kunyanyaswa na mmewe na kupata matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua zikiongezeka. Aidha, afisa huyo ameongeza kuwa jamii nzima hupoteza kutokana na ndoa hizo, kwa sababu ni chanzo cha mzunguko wa umasikini.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpae, dw
Mhariri: Josephat Charo