UNICEF: Njaa yatishia maisha ya watoto milioni 1.4
21 Februari 2017Takriban watoto milioni 1.4 kutoka Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen wanateseka kutokana na utapiamlo uliokithiri na wanaweza kufariki mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.
Katika taifa la Sudan Kusini, zaidi ya watoto 270,000 wanakumbwa na utapiamlo. Baa la njaa limeshatangazwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo mfano eneo la kaskazini ambako wanaishi watoto 20,000. Idadi ya watu wasiokuwa na usalama wa chakula nchini humo inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 5.5 ifikapo mwezi Julai endapo hakutachukuliwa hatua za kuzuia kuenea kwa ukosefu wa chakula na makali yake.
Mkurugenzi wa Shirika la Unicef Anthony Lake amehimiza juhudi za dharura zichukuliwe ili kunusuru maisha ya watoto walioko katika hatari. Mratibu katika shirika la hali ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Eugene Owuso nchini Sudan Kusini anasema mambo mengi yamechangia kukithiri kwa njaa. "Mgogoro wa ukosefu wa chakula leo hii, umechangiwa pakubwa na mapigano, ukosefu wa usalama na watoaji misaada kukumbwa na changamoto ya kufikia maeneo yaliyoathiriwa. Pia huchangiwa pakubwa na mashambulio dhidi ya watoaji misaada mbali na wizi wa misaada inayotolewa."
Migogoro na njaa
Nchini Yemen ambako kumekuwa na vita kwa muda wa takriban miaka miwili sasa, watoto 462,000 wanakabiliwa na mateso ya utapiamlo. Katika mashariki mwa nchi ya Nigeria, watoto 450,000 wamedhoofishwa na utapiamlo.
Nchini Somalia, ukame umewaacha watoto 185,000 katika hatari ya njaa huku UNICEF ikisema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka na kufikia watoto 270,000 katika miezi michache ijayo.
Mfumo wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu njaa maarufu kama Fews Net umeeleza kuwa tangu mwaka uliopita, makali ya njaa yameathiri mkoa wa Borno nchini Nigeria na janga hilo huenda litaendelea kwani mashirika ya kutoa misaada hayawezi kufika katika maeneo hayo.
Mabalozi wa Baraza Usalama la Umoja wa Mataifa, wanatarajiwa kuzuru kaskazini mwa Nigeria, Cameroon, Chad na Niger mwezi ujao kama hatua ya kuteka mawazo ya kimataifa kuhusu mgogoro wa kibinadamu ambao umesababishwa na mgogoro na wapiganaji wa kiislamu wa itikadi kali wa Boko Haram.
Mwandishi: John Juma/AFP/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman