1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF yaomba dola bilioni 9.3 za kusaidia watoto 2024

16 Desemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto ulimwenguni UNICEF, limetoa ombi la ufadhili fedha dola bilioni 9.3 ili waweze kuwafikia watoto waliokumbwa na majanga ya kibinadamu duniani kote ifikapo 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Jumatatu, Oktoba 30, 2023.Picha: Eduardo Munoz Alvarez/AP/picture alliance

Mnamo mwaka 2024, watoto ulimwenguni kote wanatarajiwa kuhitaji msaada wa kibinadamu ili kuwaokoa dhidi ya vitendo vya ukatili, umaskini, ubaguzi, na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

UNICEF imeitaja Afghanistan kuwa ndio nchi itakayohitaji gharama kubwa zaidi, huku ikitoa wito wa dola bilioni 1.4 kwa mwaka 2024, ili waweze kuwafikia watoto milioni 94 katika nchi 155.

Ustawi wa watoto duniani ni moja ya vipaumbele vya UNICEF mwaka 2024.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Miradi mingine iliyoorodheshwa katika harakati za kutafuta wafadhili ili kukabiliana na ongezeko la kutisha la idadi ya watoto wanaokabiliwa na majanga ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa duniani kote, ni pamoja na ile yaSudanna Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma zaidi: Watoto milioni 4 wahitaji msaada wa kitu Pakistan - UNICEF

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, mamilioni ya watoto wanaendelea kufikwa na majanga ya kibinadamu ambayo yanazidi kuongezeka na kuwa magumu zaidi. Catherine ameongeza kusema kuwa watoto hawapaswi kugharimika kwa maisha yao ya sasa na ya baadae, kutokana na migogoro, majanga ya asili au mabadiliko ya tabia nchi. 

UNICEF imesema ufadhili huo utaiwezesha kuwafikia watoto milioni 17.3 wanaohitaji chanjo ya surua, watoto milioni 7.6 wenye utapiamlo mkali, na watoto milioni 19.3 ambao hawana fursa ya kupata elimu.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yatoa wito zaidi

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani UNFPA, limetoa wito wa ufadhili wa dola bilioni 1.2 ili kukabiliana na matatizo yanayoongezeka yanayoathiri wanawake na wasichana duniani kote mwaka 2024.

Katika taarifa yake Mkurugenzi wa UNFPA Natalia Kanem amesema shirika hilo linalenga kuwafikia wanawake, wasichana na vijana milioni 48 katika nchi 58, kwa mwaka 2024 na wameweka vipaumbele vyao kwa nchi mbalimbali zikiwemo Afghanistan, Sudan, Yemen, Syria, Somalia na Ethiopia, ili kuwanusuru na madhara zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia, ndoa zaidi za utotoni, na vifo vingi vintokanavyo na uzazi.

Wanawake wa Tigray waliokimbia vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, wananyonyesha watoto wao ndani ya hema la UNICEF, wakati Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi, alipotembelea kambi ya wakimbizi ya Umm Rakouba huko Qadarif, Sudan Mashariki.Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

Akihutubia ufunguzi wa Kongamano la siku tatu la Kimataifa la Wakimbizi mjini Geneva, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi alitoa wito kwa wafadhili huku akisema mashirika ya misaada ya kibinadamu yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha ili kukabiliana na mizozo mingi duniani. Huku akionesha wasiwasi wao kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mwaka ujao 2024.

Grandi pia amesema Idadi ya watu walioyakimbia makazi yao na kuishi kama wakimbizi duniani kote imefikia milioni 114 hadi mwisho wa Septemba, huku akiitaja kuwa ni idadi kubwa zaidi. Kamishna huyo ametoa wito wa kuunganisha nguvu ya pamoja na kuhakikisha kwamba wale wanaokimbia kwa sababu maisha, uhuru na usalama wao uko hatarini, wanapataulinzi, na kutatua changamoto zao haraka iwezekanavyo.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW