1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Wanawake milioni 230 ni manusura wa ukeketaji

Sylvia Mwehozi
8 Machi 2024

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la UNICEF inaonyesha kuwa zaidi ya wanawake milioni 230 duniani kote ni manusura wa ukeketaji. Ongezeko hilo limechangiwa na ukuaji wa idadi ya watu katika nchi fulani.

Ethiopia-Ukeketaji
Ngariba wa zamani wa EthiopiaPicha: Holt/UNICEF/dpa/picture alliance

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la UNICEF inaonyesha kuwa zaidi ya wanawake milioni 230 duniani kote ni manusura wa ukeketaji. Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 15 tangu mwaka 2016, licha ya maendeleo katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo kwenye baadhi ya nchi.

Ripoti hiyo imetolewa ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wanawake duniani. Afŕika imekuwa na idadi kubwa zaidi ya wahanga wa ukeketaji ikiwa na zaidi ya wanawake milioni 144, mbele ya Asia milioni 80 na Mashariki ya Kati milioni sita, kulingana na utafiti wa nchi 31 ambako kunafanyika ukeketaji.

Ongezeko hilo limechangiwa na ukuaji wa idadi ya watu katika nchi fulani lakini ripoti hiyo pia iliangazia maendeleo yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya ukeketaji kwenye maeneo mengine.