UNICEF:Watoto 435 wameuwawa Sudan tangu kuzuka kwa vita
24 Julai 2023Kaimu mkurugenzi mtendaji wa UNCEF Ted Chaiban katika taarifa yake amesema kwamba, katika siku mia moja za mapigano haziwezi kuelezeka namna ambavyo watoto wameathirika.
"Athri ambazo mzozo huu umekuwa nazo dhidi ya watoto haziwezi kuelezeka"
Alisema kwenye taarifa iliotolewa kwa vyombo vya habari.
Soma pia:Sudan yatimiza siku 100 za mapigano
Kwa jumla, shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto limepokea visa 2,500 vya ukiukwaji wa haki za watoto hadi sasa, lakini taarifa inasema kwamba idadi hiyo ina uwezekano kuwa juu zaidi ya visa vilivyorekodiwa.
Kila siku watoto wanauawa, kujeruhiwa, kutekwa nyara na kushuhudia shule, hospitali na miundombinu muhimu ikiharibiwa vibaya au kuporwa,” alisema Chaiban, ambaye kwa sasa yuko Sudan.
Juhudi za upatanishi hazijazaa matunda.
Nchini Sudan, wanamgambo wa makamu wa rais wa zamani Mohammed Hamdan Daglo wa kikosi cha dharura RSF, wanapigana na vikosi vya kijeshi vinavyoongozwa na Rais Abdel Fattah al-Burhan.
Msururu wa matukio ya upatanishi, yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani, tangu kuzuka kwa mapigano mnamo mwezi Aprili, umeshindwa kuleta suluhu, huku mzozo wa kiutu ukiongezeka.
Soma pia:Mzozo wa Sudan hauna dalili za kumalizika
Wiki chache zilizopita Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan, wameonyesha dhamirayao ya kuumaliza mzozo nchini Sudan na kupeleka misaada ya kibinadamu.
Serikali ya Misri, ambayo kihistoria ina mahusiano ya karibu na jeshi la Sudan, nayo ilijitosa kwa kuwaalika wakuu wa mataifa jirani ikiwemo Ethiopia, kwa ajili ya kujadili namna ambayo inaweza kumaliza mzozo huo ambao umesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makaazi yao na wengine maelfu kuuwawa.