1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Union Berlin kumkabili Kruse ugenini Wolfsburg

Josephat Charo
3 Machi 2022

Union Berlin wanasafiri ugenini kukwaana Wolfsburg katika mechi ya 25 ya msimu wa 59 wa Bundesliga Jumamosi (05.03.2022) Mshambuliaji wa zamani wa Union Max Kruse atacheza dhidi ya klabu yake ya zamani.

Fussball 1.Bundesliga, Eintracht Frankfurt - VfL Wolfsburg
Picha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Kocha wa klabu ya Union Berlin Urs Fischer amekataa kusema lolote kuhusu kumkabili mshambuliaji wa zamani wa timu yake Max Kruse katika mechi ya Bundesliga ugenini Wolfsburg Jumamosi.

"Nafikiri yamezungumzwa ya kutosha kuhusu suala hili. Sitalizungumzia. Muhimu ni kukubali changamoto ya Wolfsburg na Max ni sehemu ya mchezo wao," Fischer aliwaambia waandishi habari Alhamisi.

Katika hatua ya kushangaza, Kruse aliondoka Union kuhamia Wolfsburg mwezi Januari mwaka huu, bila kuficha kwamba alikuwa atapata fedha nyingi huko na pia kuonesha ukosoaji wa miezi yake ya mwisho Berlin.

Union ilipoteza mechi tatu bila kufunga bao baada ya Kruse kuondoka lakini hatimaye wakarejea katika fomu yao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Mainz wikendi iliyopita na siku ya Jumanne wakafanikiwa kufuzu kwa nusu fainali ya kombe la shirikisho la Ujerumani kwa kuwazidi nguvu St Pauli Hamburg 2-1.

Union wamesema hakuna kipengee katika mkataba wa Kruse ambacho kingemzuia kucheza dhidi yao, huku msemaji wa klabu hiyo, Christian Arbert, akisema usimamizi wa klabu haujapoteza hata fikra kusisitiza juu ya kifungu kama hicho.

(dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW