1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Union Berlin waendelea kupaa kileleni mwa ligi

19 Septemba 2022

Nani alisema Bundesliga inatabirika? Hizi ni nyakati za kushangaza katika ligi kuu ya kandanda Ujerumani. Union Berlin wameingia katika kipindi cha mechi za kimataifa wakiwa kileleni mwa Bundesliga

Bundesliga | 1. FC Union Berlin - VfL Wolfsburg
Picha: JOHN MACDOUGALL/AFP/Getty Images

 Mshambuliaji wa Kimarekani Jordan Pefok na Mholanzi Sheraldo Becker walifunga tena jana na kuirudisha Union Berlin kileleni mwa ligi kwa ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Wolfsburg. Kocha wa Union Urs Fischer ambaye aliiongoza timu hiyo kupandishwa daraja mwaka wa 2019 na kusimamia muendelezo wake mwaka baada ya mwingine katika Bundesliga hata hivyo amesema vijana wake hawapaswi kuzembea kwa kuhisi kuwa wako kileleni mwa ligi na pointi 17.

Bayern walisherehekea Oktoberfest baada ya kichapoPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Mabingwa mara 10 mfululizo Bayern Munich walishiriki katika maonyesho ya kitamaduni ya bia maarufu kama Oktoberfest jana lakini sio sherehe ambayo timu hiyo ilitaka kuwa nayo baada ya kuchapwa 1 – 0 na Ausgburg Jumamosi. Sasa wamecheza mechi nne mfululizo za ligi bila kupata ushindi. Julian Nagelsmann alikuwa na haya ya kusema. "Ni vigumu kupata maneno ya kutumia leo. Mwisho wa siku, nadhani tulipotea kidogo katika kipindi cha kwanza. Lakini kuna nyakati ambazo tungefanya vizuri zaidi katika upande wa mpinzani uwanjani na hatukufurahishwa na hicho. Ni kama tulikuwa na na nafasi nyingi sana lakini tuliishiwa na muda tu."

Nahodha na kipa wa Bayern Manuel Neuer, nusra aifungie timu yake bao la kusawazisha katika dakika ya mwisho ya mchezo lakini mpira wa kichwa aliopiga ulipanguliwa na kipa wa Augusburg Rafael Gikiewicz. Gickiewicz bila shaka alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na alikuwa na haya ya kusema baada ya kuokoa mpira wa Neuer. "Nilizungumza nae baada ya mechi na kumuuliza, ulikuwa unafanya nini mwenzangu? akasema alitaka kufunga bao na akasema alifanya kitu sawa na hicho dhidi ya Inter Milan. Bahati nzuri, nilikuwa katika nafasi nzuri na nikapangua. Ni jamaa mkubwa na alipiga kichwa safi. Lakini nilitumia mkono wangu wa kushoto na kuupangua mpira."

Moukoko aliweka historia katika derby ya RuhrPicha: David Inderlied/dpa/picture alliance

Bayern wako nafasi ya tano na pointi 12. Licha ya mwanzo huo wa kusuasua wa msimu, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bayern Oliver Kahn amesema kocha Nagelsmann hapaswi kuwa na wasiwasi na kazi yake. Amesema wanamwamini na kwa sasa hawazungumzi na kocha mwingine kuhusu uwezekano wa kumpa kazi.

Kando na derby hiyo ya Bavaria, kuna mama ya debi zote Ujerumani ambapo kinda Youssoufa Moukoko ndiye alikuwa shujaa katika dimba la Signal Iduna Park lililokuwa limefurika hadi pomoni. Akiwa na umri wa miaka 17 na siku 301, Moukoko aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga katika derby ya Dortmund na Schalke. Aliingia kama nguvu mpya kuchukua nafasi ya Antony Modeste na akaifungia BVB bao hilo pekee la ushindi katika dakika ya 79.

Dortmund wako nafasi ya pili na pointi 15 mbele ya nambari tatu Freiburg ambao wana pointi 14 baada ya kutoka sare ya kutofungana bao na Hoffenheim. Hoffenheim wanashikilia nafasi ya nne na pointi 13.

afp, dpa, ap

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW