1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester United yaangukia pua Ujerumani

21 Septemba 2023

Bayern Munich, Arsenal, Real Madrid na Salzburg zatamba kwenye mechi zao za ufunguzi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya. Bundi bado anaizonga zonga Manchester United

Champions League / Bayern München - Manchester United
Nyota wa Bayern Munich Harry Kane akijifua wakati wa mchezo dhidi ya Manchester United.Picha: Sven Hoppe/picture alliance/dpa

Mechi za ufunguzi za ligi ya mabingwa barani Ulaya zimeendelea usiku wa jana ambapo mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani Bayern Munich wamezidi kuwatia unyonge mashetani wekundu, Manchester United kwa kuwachabanga mabao 4-3 katika uwanja wa Alianz Arena mjini Munich.

Soma zaidi: Mechi za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza leo

United walikwenda Ujerumani baada ya matokeo mabaya, huku wakikabiliwa na matatizo mengi nje ya uwanja na hawakupewa afueni hata kidogo na timu ya Bayern ambayo sasa imeshinda mechi 20 zilizopita za ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa.

Hali bado ni tete kwa Erik Ten Hag

Kilikuwa kipigo cha nne katika mechi sita pekee kwa vijana hao wa Erik ten Hag walioboranga katika michuano yote msimu huu huku wakishindwa kujinasua kutokana na kipigo cha aibu cha 3-1 dhidi ya Brighton wikendi iliyopita kwenye Ligi ya Premia.

Bayern walichukua udhibiti baada ya mlinda mlango mgeni Andre Onana kuruhusu shuti dhaifu la Leroy Sane kutinga wavuni dakika ya 28 kabla ya Serge Gnabry kufunga la pili. Rasmus Hojlund alifunga bao moja kabla ya Kane kufunga penalti mapema katika kipindi cha pili.

Soma zaidi : Rais wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania Luis Rubiales ajiuzulu

Jaribio la dakika za lala salama la Casemiro liliwapa United matumaini ya uwezekano wa kurejea katika mchezo, lakini mchezaji wa akiba wa Bayern Mathys Tel aliwafungia wenyeji bao la nne katika muda wa nyongeza.

Mbrazil Casemiro alifungi United bao lingine la kufutia machozi kutokana na shambulizi la mwisho la mechi hiyo. Bayern ambao ni mabigwa mara sita wa Ulaya walipanda kileleni mwa jedwali la Kundi A baada ya sare ya awali ya 2-2 Jumatano kati ya Galatasaray na FC Copenhagen mjini Istanbul.
 
Wakati Manchester wakichezea kichapo mbele wa Bayern, timu nyingine ya Uingereza, Arsenal,  imerejea katika Champions League baada ya miaka sita kwa ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya PSV Eindhoven ya uholanzi.

Arsenal yarejea kwa kishindo UEFA

Arsenal imeshinda kutokana na mabao ya kipindi cha kwanza ya Bukayo Saka, Leandro Trossard na Gabriel Jesus, na Martin Odegaard zikiwa zimesalia dakika 20.

Nyota wa Arsenal Bukayo Saka akishangilia goli lake la kwanza kwenye michuano ya UEFA baada ya kuifungia timu yake ya arsenal dhidi ya PSVPicha: Andre Boyers/AP/picture alliance

Mara ya mwisho Arsenal ilipocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ilichapwa jumla ya mabao 10-2 na Bayern Munich, wakati nafasi yao ya kudumu miongoni mwa timu nne bora za Ligi Kuu ya Uingereza ilipogeuka ya jambo la kukumbuka.

Soma zaidi: UEFA: Wachezaji nyota kuhamia Saudia isilete hofu Ulaya

Nafasi ya pili nyuma ya Manchester City msimu uliopita imewarudisha kwenye champions League na PSV ya Uholanzi imedhihirisha kuwa wapinzani wazuri katika usiku ulionyeshewa mvua kaskazini mwa London.

Washindi wa pili wa msimu uliopita Inter Milan wamefanikiwa kutoka sare ya 1-1 na Real Sociedad katika Kundi D ambapo Salzburg ndio vinara kundi hilo baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Benfica iliyokuwa na wachezaji 10. 

Mabeki wa Union Berlin ya Ujerumani wakijaribu kumzuia nyota wa Real Madrid RodrygoPicha: Manu Fernandez/AP Photo/picture alliance

Brais Mendez aliwaweka wenyeji mbele mapema lakini Lautaro Martinez aliisawazishia Inter ambao kadi yao nyekundu iliyotolewa kwa Nicola Barella ilifutwa.

Mabingwa wa Italia, Napoliwalipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Braga na kuongoza Kundi C mbele ya Real Madrid ambao waliokolewa tena na Jude Bellingham katika dakika za lala salama kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya washiriki wa mara ya kwanza wa michuano hiyo Union Berlin ya Ujerumani.

Galatasaray ya uturuki ilipambana kutoka nyuma kwa mabao mawili na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Copenhagen ya Denmark iliyokuwa na wachezaji 10 katika hatua za mwisho, huku Sevilla na Lens zilitoka sare ya 1-1.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW