1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Union wateleza, Bayern wawanyatia

24 Oktoba 2022

Vinara wa Bundesliga Union Berlin hapo Jumapili walipata pigo katika azma yao ya kutaka kuendelea kusalia kileleni mwa ligi baada ya kulazwa 2-1 na VfL Bochum huko mjini Bochum.

Fußball Bundesliga | VfL Bochum - Union Berlin
Picha: Sebastian Räppold/Matthias Koch/IMAGO

Bochum ambao wako katika hatari ya kushushwa daraja walifunga goli katika kila kipindi cha mechi hiyo na kupata ushindi wao wa pili msimu huu uliowaondoa kutoka mkiani mwa jedwali.

Kwa upande wa Union, hii ndiyo iliyokuwa mechi ya pili msimu huu waliyoipoteza.

Wachezaji wa Bochum wakisherehekea goli dhidi ya Union BerlinPicha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Dortmund yavuna ushindi mkubwa

Timu iliyovuna ushindi mkubwa mwishoni mwa wiki lakini ni Borussia Dortmund ambayo iliibamiza VfB Stuttgart 5-0 katika uwanja wa Signal Iduna Park. Kocha Edin Terzic alikuwa na haya ya kusema baada ya mpambano huo.

"Ndiyo tulitaka ushindi wa kuridhisha nyumbani. Kutokea mwanzo wa mechi tulikanyaga mafuta na hatukuuondoa mguu kamwe. Kilichoturidhisha ni kwamba magoli yote tuliyoyafunga yalikuwa magoli yaliyoishirikisha timu nzima. Tulishirikiana vyema katika kila hali, wachezaji wawili au watatu waliugusa mpira kabla pasi ya mwisho katika eneo la adhabu na ndio maana tumeridhika sana na jinsi tulivyopata magoli haya. Ushindi wa 5-0 ni mzuri sana kwetu leo lakini tunafahamu kilichotokea wiki iliyopita kwa hiyo hatutatekwa na furaha, tutauchukulia ushindi huu kama mwanzo tu na ni matumaini yetu tutaendelea vivi hivi," alisema Terzic.

Nao Bayern Munich walikuwa ugenini wakicheza na TSG Hoffenheim ila waliwazidi nguvu kwa magoli ya Jamal Musiala na Eric Maxim Choupo Moting ambaye kwa sasa hivi ni moto wa kuotea mbali. Huyu hapa kocha wao Julian Nagelsmann.

Kocha wa Bayern Munich Julian NagelsmannPicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

"Tungefunga mabao mengi zaidi kutokana na nafasi za wazi zilizojitokeza ila mabao mawili ilikuwa hatari kwasababu mpinzani wetu angefunga bao moja tu basi angerudi mchezoni. Lakini tumeshinda na ndio maana nimeridhika leo," alisema Nagelsmann.

Christopher Nkunku afunga goli la 8 msimu huu katika Bundesliga

Na katika mchuano ambao ulisisimua mno, RB Leipzig walitoka chini magoli matatu kwa bila na kunako dakika za mwisho wakayasawazisha magoli yote na mechi yao na Augsburg ikaishia mabao 3-3.

Andre Silva na Christopher Nkunku aliyefunga mkwaju maridadi kabisa wa penalti na kuhakikisha kwamba anakwea hadi kileleni mwa wafungaji bora wa Bundesliga msimu huu akiwa na magoli 8, walikuwa miongoni mwa wafungaji.

Kocha wa Augsburg Enrico Maaßen alizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi.

"Kwanza lazima niseme timu yangu imecheza vizuri sana hadi pale kulipotolewa kadi nyekundu ambayo ilikuwa sahihi. Hadi hapo tulikuwa tunacheza kwa kujituma mno. Nafikiri ukiwa unaongoza kwa mabao mawili hadi kuelekea mwisho mwisho wa mchezo kukiwa kumesalia dakika mbili tu, unastahili kutumia ala zako zote kujilinda. kwa hiyo kwa leo hatujaridhika na pointi moja bila shaka na lazima turekebishe hilo ila tukiwa nyumbani na unaongoza kwa mabao 3-0 na ukiwa umeingia uwanjani baada ya mpinzani wako kuwa na mapumziko ya siku moja zaidi, basi kwetu ni jambo la kujivunia," alisema Maaßen.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW