1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNITA na uchaguzi ujao Angola

17 Aprili 2008

Kiongozi wa UNITA Samakuva atahadharisha na kusisitiza juu ya haja ya amani na utulivu kuepusha yaliotokea Kenya na Zimbabwe.

Rais dos Santos na kiongozi wa zamani wa UNITa Jonas Savimbi(koti jeupe) baada ya kusaini makubaliano ya amani Mei 6, 1995 mjini Lusaka Zambia.Katikati ni rais wa zamani wa Zambia Frederick Chiluba. Makubaliano hayo hayakudumu na Savimbi akarudi msituni.Picha: AP

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Angola UNITA Isaias SAMAKUVA ametahadharisha kuwa uchaguzi ujao wa bunge utakaokua wa kwanza katika kipindi cha miaka 16 baada ya miaka 27 ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe unapaswa kuwa huru na haki kuepusha matokeo sawa na yale ya Kenya au Zimbabwe. Lakini akasisitiza ana imani utakua wa utulivu.

Kiongozi huyo wa Unita alikua akizungumza katika mji mkuu wa Ureno Lisbon na kusema haoni sababu ya kutokea vuta nikuvute sana ya Zimbabwe wakati huu au umwagaji damu uliotokea Kenya baada ya uchaguzi wa Desemba mwaka jana. Akasisitiza ana imani hiyo kutokana na uzoefu wa Angola wa vita vya miaka mingi vilivyoivuruga nchi hiyo.

Angola ni nchi ya pili kubwa kwa utoaji mafuta baada ya Nigeria katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara na inatarajia kufanya uchaguzi wake wa bunge mkuu tarehe 5 na 6 Septemba na ule wa rais kufuata mwaka ujao.

Bw Samakuva mwenye umri wa miaka 62 na aliyechukua hatamu za uongozi wa Unita 2003 mwaka mmoja baada ya kusaniwa mkataba wa kusimamisha mapigano, amesema nia ya waangola ni kuimarisha demokrasia, baada ya karibu miongo mitatu ya vita.

Chama tawala MPLA kinachoiongoza Angola tangu uhuru kutoka kwa Ureno 1975, kwa hivi sasa kina wingi bungeni kikiwa na viti 129 kati ya 220, wakati Unita kina viti 70

Akizungumzia imani yake kwamba uchaguzi ujao utakua huru na maamuzi ya wapiga kura kuheshimiwa, Bw Samakuva alisema kuna hali ya kuridhisha kuweza kuwa na uchaguzi wa amani na utulivu.

Akaitaka jumuiya ya kimataifa kutokua na wasi wasi wowote na alikua pia na wito kuhusiana na utaratibu wa uchaguzi,"Jumuiya ya kimataifa siwe na wasi wasi wowote na Unita kuhusiana na uchaguzi ujao, kwa sababu ni mshirika wa kuaminika. Lakini tunaiomba jumuiya ya kimataifa ijihusishe kiakamilifu katika mwenendo mzima wa kuangalia uchaguzi huo. Kwa mtazamo wetu kunapaswa kuweko na jumla ya waangalizi 70,000 katika uchaguzi huo ili kufanikisha zoezi hilo kwa amani na bila ya matatizo yoyote."

Angola haikua na uchaguzi 1992, ulipozuka mgogoro kuhusu uchaguzi wa rais na kiongozi wa Unita wakati huo Jonas Savimbi kuamua kurudi tena msituni, aliposhindwa na rais wa sasa wa Angola na kiongozi wa MPLA Jose Eduardo dos Santos.

Kifo cha Savimbi wakati wa mapigano na majeshi ya serikali 2002, ndicho kilichokua chanzo cha kumalizika vita hivyo vilivyowauwa watu karibu ya milioni moja , maelfu kuwa vilema kutokana na mirupuko iliotegwa ardhini, na pia kuharibu sehemu kubwa ya miundo mbinu nchini humo zikiwemo barabara .

Rais Eduardo dos Santos mwenye umri wa miaka 67, anaitawala Angola kwa miaka 30 sasa na anatarajiwa bado kuwa mgombea wa MPLA katika uchaguzi ujao wa rais, licha ya taarifa za vyombo vya habari nchini humo kwamba hali yake ya afya si nzuri. Lakini kwa upande wake Bw Samakuva amedhibitisha atakua mgombea akiwa mpinzani mkuu wa rais dos Santos. Alipoulizwa alisema,"Bila ya Shaka."

Baada ya miaka sita ya amani, nchi za magharibi na mataifa yanayoinukia kuwa nguvu kubwa kiuchumi kama China yameigeukia Angola yakijiingiza katika sekta ya mali asili na hasa mafuta na madini, kupiga jeki ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo. Angola itafungua soko la fedha mwaka huu, kuruhusu wawekezaji kuchangia katika utajiri wake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW