1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN:Libya huenda ikawa na serikali mbili

17 Machi 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya siasa, Rosemary DiCarlo ametahadharisha kuwa Libya huenda ikajikuta ina serikali mbilihali itakayosababisha nchi hiyo kurejea katika machafuko

USA | UN Sicherheitsrat in New York zur Lage in Äthiopien
Picha: Manuel Elias/Xinhua/picture alliance

 

DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ametoa wito kwa Libya kufanya uchaguzi haraka iwezekanavyo ili kuliunganisha taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Aidha, DiCarlo amesema anatiwa moyo na hatua ya umoja wa mataifa ya kuunga mkono juhudi za kuanzisha kamati ya pamoja ya Baraza la Wawakilishi la Libya na Baraza Kuu la Kitaifa kwa lengo la kufikia makubaliano baina ya pande hizo hasimu, kwa misingi ya kikatiba ambayo itasababisha uchaguzi kufanyika mwaka huu.

Kutofanyika uchaguzi chanzo cha mvutano

Mgogoro ulizuka baada ya Libya kushindwa kufanya uchaguzi wake wa kwanza wa rais uliotarajiwa kuandaliwa Desemba 24 chini ya upatanisho unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Baraza la Wawakilishi lenye makao yake mashariki mwa Libya lilimtaja waziri mkuu mpya, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Fathi Bashagha, kuongoza serikali mpya ya mpito mwezi Februari.

Abdul Hamid Dbeibah na Fathi BashaghaPicha: picture-alliance

Soma zaidi:Umoja wa Mataifa wajitolea kupatanisha Libya

Wabunge hao walidai kwamba mamlaka Waziri Mkuu wa muda Abdul Hamid Dbeibah, ambaye makao yake ni mji mkuu, Tripoli, yaliisha wakati uchaguzi uliposhindwa kufanyika.

Lakini Dbeibah anasisitiza kuwa atasalia kuwa waziri mkuu hadi uchaguzi utakapofanyika, na Baraza Kuu la Jimbo, ambalo linashauri serikali ya mpito limeutaja uamuzi wa bunge kufanya uchaguzi wakumtaja waziri mkuu mpya sio sahihi.

DiCarlo amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya, Stephanie Williams amejitolea kuwa mpatanishi kati ya Abdul Hamid Dbeibah na Fathi Bashagha ili kuondoa mkwamo wa sasa wa kisiasa.

Umoja wa Mataifa waingilia kati

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Stephanie Williams, amemuomba spika wa Baraza la Wawakilishi na rais wa Baraza kuu la Jimbo kuteua wajumbe sita kwenye kamati ya pamoja na wote wawili waliitikia mwito wake.

Libya ilitumbukia katika machafuko baada ya uaasi ulioungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO mwaka 2011 uliopelekea kupinduliwa kwa dikteta wa muda mrefu Moammar Gadhafi.

Soma zaidi:Kizungumkuti cha serikali mpya nchini Libya

Taifa hilo kwa miaka mingi, limegawanywa kati ya tawala pinzani za mashariki na magharibi, kila moja kuungwa mkono na safu ya wanamgambo na serikali za kigeni.