1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unyakuaji "Ukingo wa Magharibi" huenda ukawa mgumu

11 Juni 2020

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huenda akakakumbana na ugumu katika utekezaji wa unyakuzi kwenye Ukingo wa Magharibi, wakati mjadala rasmi wa baraza la mawaziri ukitarajiwa kuanza Julai Mosi.

Israeli Kabinettsitzung | Benjamin Netanjahu
Picha: Reuters/A. Sultan

Baraza la mawaziri la Israel limesema waziri mkuu Benjamin Netanyahu bado hajafanikiwa kupunguza tofauti kati yake na Marekani pamoja na mshirika wake muhimu katika serikali ya muungano kuhusiana na ahadi yake ya kuyanyakua baadhi ya maeneo kwenye Ukingo wa Magharibi. 

Matamshi hayo yaliyotolewa na waziri wa masuala ya makazi wa Israel Tzipi Hotovely yaliangazia ugumu ambao Netanyahu huenda akakakumbana nao katika utekezaji wa hatua hiyo katika eneo wanalolikalia hivi karibuni, wakati mjadala rasmi wa baraza la mawaziri ukitarajiwa kuanza Julai Mosi.

Sambamba na mpango wa amani wa Mashariki ya Kati uliotangazwa na rais Donald Trump wa Marekani mwezi Januari, Netanyahu alisema anafikiria kutanua mamlaka ya Israel kwenye makazi ya walowezi wa Kiyahudi na bonde la Jordan lililopo kwenye Ukingo wa Magharibi.

Wapalestina wanalitaka eneo hilo, pamoja na Gaza na Jerusalem Mashariki kwa ajili ya kuunda taifa lao.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa kwenye moja ya vikao vya baraza la mawaziri.Picha: Reuters/M. Kahana

Wametoa mwito wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Israel, na mataifa ya Kiarabu na Ulaya yameelezea wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo ya upande mmoja ya kugawa mipaka kwamba inaweza kuhujumu mchakato wa suluhu ya mataifa mawili kufuatia mzozo uliodumu kwa muda mrefu. 

Hotovely amekiambia kituo cha redio ya jeshi kwamba kuna tofauti kati ya Wamarekani na Israel kuelekea suala hilo, lakini pia miongoni mwao wenyewe na washirika wao waandamizi katika serikali ya muungano na chama cha Blue na Nyeupe, akiangazia mwito wa majadiliano mapana ya kimataifa uliotoloewa na chama hicho kinachoongozwa na waziri wa ulinzi Beny Gantz, kuhusiana na suala hilo.

Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya huko Palestina Sven Kühn von Burgsdorff alisema, iwapo maeneo hayo yatanyakuliwa, itaathiri mahusiano kati ya Israel na umoja huo.

Hapo jana, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Heiko Maas akiwa Jordan alitoa mwito wa majadiliano ya kina kati ya Israel na Palestina. Alisema alipokuwa akifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Jordan Ayman Safadi, akitokea Israel, ambako alielezea wasiwasi mkubwa iwapo hatua hiyo itatekelezwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas akiwa na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/photothek/F. Gaertner

"Tumeashiria kwamba sasandiyowakati wa diplomasia na majadiliano, huu ni wakati muhimu. Huu sio muda wa kutishiana. Nimezungumza na pande zote leo na ninajaribu kutafuta njia ya kuwa na msingi ama makubaliano ya pamoja, hata kama inaonekana kuwa ni ngumu." alisema Maas.

Soma Zaidi: Ujerumani yaonya dhidi ya unyakuzi wa Israel.

Waziri Safadi kwenye mazungumzo hayo alipinga vikali unyakuaji wa maeneo hayo, kwa kuwa hilo litaua kabisa suluhu ya mataifa mawili, kudhoofisha msingi wa mchakato wa amani na kuwanyima haki ya kuishi kwa amani raia wa ukanda mzima.

Mwezi uliopita mfalme wa Jordan Abdullah II aliliambia gazeti la Ujerumani la Der Spiegel kwamba hatua ya Israel ya kuyanyakua maeneo hayo itatishia kuibua mzozo na taifa lake, matamshi yanayoungwa mkono na Maas ambaye anasema Jordan kama jirani wa karibu itaathirika zaidi kuliko mataifa mengine kwa hatua yoyote itakayochukuliwa.

Mashirika: RTRE/AFPE.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW