Unyanyasaji wa wanawake uadhibiwe vikali zaidi
15 Aprili 2008Katika mkutano wake wa mwaka mjini Vienna, Austria Halmashauri ya Umoja wa Mataifa kuzuia Uhalifu, imeongezea kuwa visa vya kuwadhalilisha wanawake hasa hukutikana katika maeneo ya migogoro.Halmashauri hiyo ya Umoja wa Mataifa inazitaka serikali zichukue hatua zaidi kuzuia udhalilishaji wa wanawake na wasichana.Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Madawa na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa,Antonio Maria Costa alipofungua mkutano wa Vienna alisema,nchi zenye serikali dhaifu huathirika zaidi kwa uhalifu.Vile vile wanawake wanaoishi katika nchi hizo hunyanyaswa.
Akaeleza kuwa Umoja wa Mataifa na Kamisheni ya Ulaya zinazindua miradi ya kuwasaidia wanawake waliodhaliliwa.
Kwa maoni ya msemaji wa idara hiyo ya UN Walter Kemp,ingawa nchi zinazolengwa hasa ni zile zisizokuwa na mfumo imara wa kisheria,serikali zote zinapaswa kushirikiana katika suala la kupambana na uhalifu wanaotendewa wanawake.Anasema:
"Kuna tofauti jinsi uhalifu unavyokabiliwa na mahakama. Kwa mfano uhalifu dhidi ya wanawake unahusika pia na pombe.Halafu kuna suala la mtazamo wa jamii kuelekea wanawake.Ni kweli kuwa katika baadhi ya nchi,uhalifu wa aina hiyo huadhibiwa vikali zaidi.Hata hivyo unyanyasaji wa wanawake ni tatizo la ulimwengu mzima."
Umoja wa Mataifa hutumia pesa nyingi sana katika maeneo ya mapigano kama vile Darfur nchini Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Katika maeneo hayo ya mapigano na hata kule ambako vita vimeshamalizika,mara nyingi hakuna utawala wa kisheria;rushwa na unyanyasaji ndio umetia mizizi.Madola yanayohudhuria mkutano wa Vienna yamekumbushwa kuwa msaada na haki,ni mambo yanayopaswa kwenda sambamba.
Walter Kemp anasema: "Ikiwa pesa zinazotolewa kwa misaada ya maendeleo au ukarabati huchukuliwa na wadokozi,basi kazi za ujenzi mpya hukawia na wakati mwingine hukosa kutekelezwa kabisa."
Akaongezea,kuwa wanachojaribu ni kuimarisha mfumo wa kisheria kuhusika na uhalifu hasa katika jamii zilizotoka vitani.Wanafanya kazi pamoja na mashirika ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa utawala wa kisheria ni sehemu muhimu katika misaada ya maendeleo inayotolewa.
Umoja wa Mataifa unasema,imedhihirika kuwa uhalifu ni hali inayoogopwa zaidi na watu hata kuliko vita,ugaidi,njaa au mabadiliko ya hali ya hewa.Bara Afrika linakabiliwa na vitisho vikubwa viwili.Usafirishaji wa madawa ya kulevya, silaha na binadamu katika eneo la jangwa la Sahara.Pili pia ni usafirishaji kama huo lakini pesa zinakwenda katika mikono ya waasi na magaidi.