Unyanyasaji wanawake waongezeka Gaza
29 Novemba 2024Umoja wa Mataifa umesema Ukanda wa Gaza umetumbukia katika hali ya kukosa mwelekeo huku njaa ikiongezeka, uporaji na ubakaji katika maeneo wanakojihifadhi wakimbizi. Lakini juu ya hilo ripoti za hivi punde zinasema watu wasiopungua wanane wamejeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi baada ya basi moja kushambuliwa.
Kwa kutazama kwanza kinachoripotiwa muda huu huko Ukingo wa Magharibi, kitengo cha kutowa huduma ya ukoaji cha Israel kimesema basi moja limeshambuliwa kwa kufyetuliwa risasi karibu na eneo la makaazi ya Walowezi na watu wanane wamejeruhiwa.
Machafuko yaongezeka Ukingo wa Magharibi
Machafuko yameongezeka Ukingo wa Magharibi tangu vilipozuka vita vya Gaza vilivyochochewa na shambulio la wanamgambo wa Hamas la uvamizi kusini mwa Israel,Oktoba 7 mwaka jana.
Soma pia: Marekani kuishinikiza Israel kutoshambulia maeneo ya kiutuTawi la kijeshi la kundi la Hamas la Ezzedine al Qassam limedai kuhusika na shambulio hilo ambalo limesababisha pia uharibifu wa basi hilo huku watu wanne wakijeruhiwa kwa risasi watatu kati yao wakiachwa katika hali mbaya huku wengine wakipata majeraha madogo madogo.
Lakini katika Ukanda wa Gaza Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina Ajith Sunghay, amefanya ziara kwenye maeneo kadhaa ya Gaza na kusema kwamba hali ni mbaya.
Njaa uporaji na idadi ya visa vya ubakaji yameongezeka huku utawala wa kisheria ukiwa umeporomoka.Sunghay anasema Wapalestina wanateseka kwa kiwango ambacho hakina mithili na kwamba katika ziara yake hiyo mara hii alishtushwa sana hususan na ongezeko la njaa.
Mjumbe huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameviambia vyambo vya habari Geneva kupitia mtandao akiwa Amman Jordan, kwamba walitowa tahadhari miezi kadhaa iliyopita juu ya hali ya kuporomoka kabisa kwa utawala wa sheria Gaza na hivi sasa hilo linashuhudiwa waziwazi.
Ukatili mkubwa wanafanyiwa wanawake ikiwemo ubakaji na madhila mengine katika makambi wanakojihifadhi ndani ya Gaza,lakini pia watoto wananyanyasika kwenye makambi hayo.
Wakati mgogoro huu wa Mashariki ya kati ukihusisha matukio tofautitofauti ndani ya mamlaka ya Wapalestina,nje nako yapo mengi yanayojitokeza.Soma pia: Israel yatakiwa kuondoka kwenye maeneo yote inayoyakalia kimabavu
Nje ya Gaza Wapalestina waungwa mkono
Maelfu ya watu wameandamana mjini Amman Jordan kulaani mashambilizi ya Israel Gaza huku wakiyatolea mwito mataifa ya kiarabu kuwaunga mkono Wapalestina.
Nchini Lebanon mkuu wa kundi la wanamgambo la Hezbollah Sheikh Naim Qassem anatarajiwa kuhutubia muda wowote kutoka sasa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mpango wa usitishaji mapigano na Israel siku mbili zilizopita.
Mjini Geneva Iran,Uingereza na Ujerumani zinakutana hivi sasa katika kikao kilichogubikwa na usiri mkubwa kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran chini ya kiwingu cha fukuto la mivutano kabla ya Donald Trump hajachukuwa madaraka nchini Marekani.
Katika hali ambayo sio ya kawaida mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo wamekataa kutowa ufafanuzi wowote kuhusu ajenda za mkutano huu au hata kutaja ni wakati gani unafanyika mkutano huo na wapi au utakwenda kwa muda gani.
Wasiwasi umejengeka kufuatia tamko la tahadhari iliyotolewa na mkuu wa shirika la ujasusi la Uingereza,likionesha kwamba malengo ya Nuklia ya Iran yanasababisha kitisho kikubvwa kwa usalama wa dunia, licha ya nafasi yake kudhoofika baada ya waitifaki wake Hamas na Hezbollah kupata pigo kubwa.
Richard Moore alitoa hotuba mjini Paris na huko ndiko alikosema kwamba makundi ya wanamgambo washirika wa Iran wamepata pigo kubwa kote mashariki ya kati lakini malengo ya Nuklia ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu ni kitisho kwa kila mmoja.