1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unyanyasaji wasababisha wasichana kuacha kutumia mitandao

5 Oktoba 2020

Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto na wasichana, Plan International limesema unyanyasaji wa mitandaoni umesababisha wasichana kuacha kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Aleppo Mädchen mit ihrem Mobiltelefon im Lebensmittelgeschäft
Picha: REUTERS/A. Ismail

Utafiti huo mpya uliofanywa na shirika hilo na kuchapishwa siku ya Jumapili uliwajumuisha wasichana na wanawake 14,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 kwenye nchi 22, ikiwemo Brazil, Benin, Marekani, Nigeria, Uhispania, Thailand na India. Kwa mujibu wa shirika hilo, takriban wasichana asilimia 60 wamekumbana na unyanyasaji wa mitandaoni.

Mtendaji Mkuu wa Plan International, Anne-Birgitte Albrectsen amesema wasichana wananyamazishwa kwa kunyanyaswa vibaya mitandaoni. Asilimia 39 ya wasichana walikumbana na unyanyasaji kwenye mtandao wa Facebook, asilimia 23 Instagram, asilimia 14 Whatsapp, asilimia 10 Snapchat, asilimia 9 Twitter na asilimia 6 Tiktok.

Wasichana wabadili njia ya kujieleza

Utafiti huo umegundua kuwa mmoja kati ya wasichana watano alikuwa amepunguza au ameacha kutumia kabisa mitandao ya kijamii kutokana na mashambulizi ya aina hiyo. Plan International imesema kuwa mmoja kati ya wasichana 10 alibadili njia anayoitumia kujielezea mitandaoni.

Kulingana na utafiti huo, takriban asilimia 22 ya wasichana waliohojiwa wamesema wao wenyewe au rafiki zao wamebaki na woga kuhusu usalama wao, kwani nusu ya hao wanahofia kunyanyaswa kingono au kimwili. Unyanyasaji mkubwa waliokumbana nao wasichana hao ni pamoja na kudhalilishwa kwa makusudi ambapo asilimia 41 waliathirika, asilimia 39 ya wasichana walikumbana na lugha za matusi, kuchekwa maumbile yao pamoja na vitisho vya unyanyasaji wa kijinsia. Wasichana wengi wamesema unyanyasaji huo umewaathiri kiakili.

Alama za mitandao mbalimbali ya kijamiiPicha: picture-alliance/N. Ansell

Hatua za haraka zichukuliwe

Albrectsen amezitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuchukua hatua haraka kulishughulikia tatizo hilo na amezitolea wito serikali kupitisha sheria za kukabiliana na unyanyasaji wa mitandaoni. Utafiti huo umebaini kuwa hapakuwa na maeneo sahihi ya kuripoti kuhusu kuzuia unyanyasaji huo ambao unahusisha ujumbe mbaya, picha za ngono pamoja na kuwafatilia watu kwa siri.

''Wanaharakati wakiwemo wale wanaotetea usawa wa kijinsia walilengwa mara nyingi na maisha yao na familia zao yako hatarini kutokana na vitisho wanavyopokea,'' alifafanua Albrectsen.

Mkurugenzi huyo wa Plan International ameongeza kusema kuwa kuwaondoa wasichana kwenye majukwaa ya mitandao kunawafanya kutokuwa na nguvu katika ulimwengu unaokuwa kidijitali na kunaathiri uwezo wao wa kuonekana, kusikilizwa na kuwa viongozi.

Shirika hilo la misaada limesema litaiwasilisha ripoti hiyo kwenye kampuni za mitandao ya kijamii na wabunge ulimwenguni kote na kwamba unyanyasaji huo unazikandamiza sauti za wasichana katika wakati huu wa janga la COVID-19, ambapo sauti zao zilikuwa zinahitajika. Kwenye barua yao ya wazi kwa Facebook, Instagram, TikTok na Twitter, wasichana kutoka ulimwenguni kote wamezitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuanzisha njia bora zaidi za kuripoti unyanyasaji.

(Reuters, DW https://bit.ly/3nhKU8T)