1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upande wa upinzani Zimbabwe walalamikia hatua za kuelekea uchaguzi.

27 Machi 2008

Harare.

Upande wa upinzani nchini Zimbabwe umeendelea kutoa malalamiko jana wakati jumuiya ya kimataifa inawasi wasi juu ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma hili, licha ya uhakika inaotoa serikali kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.

Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC pamoja na mgombea wa kujitegemea Simbarashe Stanley makoni wamekishutumu chama tawala cha rais Mugabe cha ZANU PF kwa kujaribu kuiba kura, wakitumia majeshi ya usalama , kuwabana wafuasi wa upinzani.

Akizungumzia hali hiyo mfanyakazi wa shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International na ambaye anaangalia hali ya uchaguzi nchini Zimbabwe kwa niaba ya shirika hilo Simeon Mawanza alisema kuwa kuna ukandamizaji usiokuwa wa lazima dhidi ya wafuasi na viongozi wa upinzani.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeshutumu kile inachokiita hali dhahiri inayotarajiwa katika hatua za uchaguzi.

Katibu mkuu wa chama cha upinzani cha MDC Tendai Biti ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hali haijawa nzuri kwa ajili ya uchaguzi huru na wa haki nchini Zimbabwe.