Upigaji kura umeanza Venezuela
30 Julai 2017Kura hiyo imekuwa ikipingwa sana katika miezi kadhaa ya maandamano mitaani na kukosolewa kimataifa.
Upinzani nchini Venezuela unasema ni juhudi za Maduro ambaye anakumbwa na matatizo kung'ang'ania madarakani kwa kuzunguka nyuma ya bunge ambalo linadhibitiwa na upinzani.
Televisheni ya taifa imemuonesha maduro akipiga kura katika eneo la magharibi mjini Caracas kwa ajili ya bunge la wananchi litakalokuwa na wajumbe 545 ambalo litakuwa na mamlaka ya kulivunja bunge linalodhibitiwa na wapinzani na kubadilisha sheria wakati likifanya mageuzi ya katiba ya nchi hiyo.
"Mimi ndie mpigaji kura wa kwanza nchini. Namuomba Mungu kwa baraka zake ili watu waweze kutimiza kwa uhuru mchakato wa haki zao za kidemokrasia na kuweza kupiga kura," rais amesema . Aliongozana na mkewe, Cilia Flores , ambaye ni mgombea ambaye atakuwamo katika bunge hilo jipya.
Idadi ya watu waliojitokeza itakuwa muhimu katika uchaguzi huo. Upande wa upinzani umetoa wito wa kususia kura hiyo, ukisema kura hiyo ni juhudi za kumuelekeza Maduro katika "udikteta" kwa kuungwa mkono na jeshi.
Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura
Uchunguzi uliofanywa na kampuni inayochunguza maoni ya wapiga kura ya Datanalisis unaonesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya watu wa Venezuela wanapinga wazo la bunge hilo jipya -- na asilimia 80 wanakataa uongozi wa Maduro.
Miezi minne ya maandamno ya mitaani dhidi ya Maduro yamesababisha zaidi ya watu 100 kuuwawa, na kuweka wazi mgawanyiko mkubwa wa kisiasa katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambalo hivi sasa limetumbukia katika hali mbaya ya kiuchumi.
Maandamano zaidi yameitishwa leo Jumapili kwa ajili ya kupinga kura hiyo, licha ya marufuku iliyotolewa na Maduro na kuamuru kitisho cha kuwaweka jela waandamanaji kwa kipindi hadi miaka 10.
Lakini hofu ya kuongezeka kwa ghasia imesambaa katika eneo hilo, na hata kupindukia.
Marekani , Umoja wa Ulaya na mataifa makubwa ya Amerika kusini , ikiwa ni pamoja na Argentina, Brazil , Colombia na Mexico zimejitokeza kupinga kura hiyo, yakisema itaharibu demokrasia nchini Venezuela.
Mashirika kadhaa ya ndege ya kimataifa , ikiwa ni pamoja na shirika la ndege la Ufaransa, Delta, Avianca na Iberia yamesitisha safari zake kwenda nchini humo kutokana na hofu ya usalama.
Familia za wanadiplomasia wa Marekani zimeamuriwa kuondoka kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya maafisa 13 wa sasa na wazamani wa Venezuela.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isacc Gamba