Upigaji kura wa mapema Zanzibar wazua minong'ono
14 Oktoba 2020Mvutano huo umetokana na Chama kikuu cha Upinzani cha ACT Wazalendo kutilia shaka upigaji wa mapema ambapo kunahitaji uwazi kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC ambayo imeweka msimamo wa kufuata sheria inayoruhusu upigaji wa kura mara mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari mwanasheria wa ACT Wazalendo Omar Said Shaaban amesema licha ya kuwaandikia barua Tume kutaka ufafanuzi na kuondoa shaka juu ya kura ya mapema lakini bado majibu hayajajitosheleza.
"Ni watu gani wataruhusiwa kulinda masanduku ya kura ya mapema yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa kanuni? kwa msisitizo tuliwauliza ZEC, watajumuisha mawakala wa vyama vya siasa?" alisema Omar Said Shaaban.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina amesisitiza kwamba tume hiyo imeandaa chaguzi mbili kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na baraza la wawakilishi ili kutoa nafasi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kupiga kura mapema. " Lakini sheria imeweka wazi kwamba tume ya uchaguzi Zanzibar inapaswa kuendesha kura siku moja kabla au siku nyingine zozote itakazoona inafaa"
Hoja ya kura ya mapema pia imegeuzwa ni ajenda kwenye majukwaa ya kampeni ambapo Maalim Seif Sharif Hamad mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo akiwataka wafuasi wake waende Oktoba 27 kupiga kura, Makamu wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwahimiza watu wake wa CCM wakapige kura Oktoba 28.
Mikutano ya vyama mbali mbali ya kampeni inaendelea huku vyama hivyo vikinadi sera zao.