Upigaji kura waendelea Marekani
3 Novemba 2020Vituo vya kura vilifunguliwa mapema leo ili Wamarekani kuchagua nani atakuwa rais wao mpya kati ya Rais Donald Trump wa chama cha Republican na Joe Biden wa Democratic. Upigaji kura ulianza katika miji miwili midogo ya Hampshire ambayo imeendelea kushikilia utamaduni wao wa kuanza kupiga kura saa sita usiku majira ya Marekani. Kwingineko, katika majimbo ya mashariki vituo vilifunguliwa saa kumi na mbili au saa moja asubuhi majira ya huko. Upigaji kura unatarajiwa kufanyika katika zaidi ya majimbo 50 ya taifa hilo.
Soma pia: Marekani kuchagua rais mpya leo
Tayari takriban watu milioni 100 walishapiga kura zao kwa njia ya posta kufuatia mpango wa upigaji kura wa mapema. Idadi hiyo kubwa ambayo ni ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika chaguzi zilizopita, ilichochewa kwa kiwango kikubwa na janga la corona, ambalo limeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 231,000 nchini humo. Wale ambao walishiriki upigaji kura wa mapema mwaka huu, ni sawa na asilimia 75 ya jumla ya waliopiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2016. Licha ya hayo bado kuna mamilioni ya watu ambao wanatarajiwa kupiga kura leo. Rais Trump aliye na umri wa miaka 74 na anayewania muhula wa pili, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mdemokrat Joe Biden. Hata hivyo Trump amesema anafikiri Warepublican watashinda. "Tunahisi vizuri sana. Tunafikiri tutashinda kwa kishindo jimbo la Texas. Tunafikiri tutashinda zaidi Florida. Tunafikiri tutapata ushindi mkubwa pia Arizona na tutafanya vizuri North Carolina na Pennsylvania. Tunafikiri tunafanya vizuri kila mahali."
Soma pia:Trump na Biden washambuliana katika kampeni Florida
Uchaguzi huo ni kama kura ya maoni dhidi ya utawala wa kujitutumua na wa msuguano wa Rais Trump ambaye mshindani wake Joe Biden amewahimiza wapiga kura kuumaliza ili kuirejesha kila anachokitaja kuwa ‘‘demokrasia yao".
Joe Biden mwenye umri wa miaka 77, ambaye pia ni makamu wa zamani wa rais, anaongoza katika kura za maoni. Hata hivyo kuna majimbo kadhaa ambako kuna ushindani mkali. Wapiga kura walio na umri wa chini ya miaka 30, ambao ndio wengi miongoni mwa waliokosa kujitokeza kupiga kura mwaka 2016, wakati huu wamejitokeza. Takriban asilimia 63 kati yao wakimuunga mkono Joe Biden.
Uchaguzi huo unafanyika mnamo wakati, taifa la Marekani limegawika zaidi na ghadhabu ni nyingi kuliko kuwahi kushuhudiwa wakati wowote tangu kipindi cha vita vya Vietnam miaka ya 1970. Soma pia: Mbivu na mbichi kujulikana kesho Marekani
Aidha kuna hofu kwamba Trump anaweza kuyapinga matokeo, hali ambayo inaweza kuzidisha taharuki. Hadi akimaliza kampeni zake jana, Trump aliendelea kudai kuwa kuna kitisho cha udanganyifu kufanywa kwenye kura hizo dhidi yake.
Warepublican wanapambana ili wapate viti vingi katika baraza la seneti ili waendelee kulidhibiti baraza hilo dhidi ya wenzao wa Wademokrat.
Suala la namna ambavyo utawala wa Trump umelishughulikia janga la corona linatarajiwa kuwa miongoni mwa hoja zitakazoshawishi namna watu watakavyopiga kura.
Miongoni mwa majimbo yenye ushindani mkali na yanayotarajiwa kutoa mwelekeo wa nani ataibuka mshindi ni Pennsylvania na Florida.
(DW, AFPE, AP, DPAE)