Upinzani Afrika Kusini wamchagua kiongozi mweusi
11 Mei 2015Hiyo ni hatua kubwa katika juhudi za DA kujitanabaisha kama mbadala kwa kile kinachotawala cha African National Congress – ANC. Chama cha Democratic Alliance – DA, ambacho kimeonekana na wengi kuwa cha wazungu wa tabaka la wastani, kilipata asilimia 22 ya kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kinalenga kuutanua mwonekano wake miongoni mwa wapiga kura weusi, ikiwa ni miongo miwili baada ya kukamilika utawala wa ubaguzi wa rangi.
Mmusi Maimane, mwenye umri wa miaka 34, alijiunga na chama cha DA mnamo mwaka wa 2009 na akapata fursa ya kujiimarisha katika chama hicho wakati Helen Zille alipojiuzulu kama kiongozi wa chama baada ya kuhudumu kwa miaka minane.
Zille hakumwidhinisha hadharani Maimane, lakini ndiye aliyepigiwa upatu kushinda uchaguzi wa chama. Akizungumza baada ya ushindi wake, Maimane alisema "Tunakubali ukweli kwamba waafrika kusini weusi kwa kiasi kikubwa wamenyimwa haki kutokana na yaliyopita. Tunakotaka kuelekea ni kuijenga jamii. Na lazima tukubali kuwa vijana pia wana matatizo. Nilisema kuwa asilimia 66 yao inajumuisha sehemu ya asilimia 35 ya wasio na ajira. Tunastahili kufanya kazi kwa bidii kuelekea hilo ili siku moja fursa zilizopo kwa Waafrika Kusini, mwishowe zitasaidia kuijenga jamii ya mchanganyiko".
Maimane alikulia katika mtaa wa Soweto, ambao ulikuwa kitovu cha vuguvugu la kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi, na akakata mizizi ya familia yake katika chama cha ANC ili kujiunga na Democratic Alliance. Mwaka jana, alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama bungeni, ambako kila mara amekuwa akikabiliana na wabunge wa ANC na Rais Jacob Zuma. Chama cha DA kimekuwa kikishinikiza kuchukuliwa hatua dhidi ya Zuma kuhusiana na tuhuma za ufisadi, na Maimane aliapa kufanikisha suala hilo.
Chama cha ANC ambacho kimetawala tangu mwaka wa 1994 wakati shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi Nelson Mandela alipochaguliwa kuwa rais wa Afrika kusini, na kinasalia kuwa chenye nguvu katika siasa za nchi hiyo, kinakabiliwa na changamoto ya uchaguzi wa mitaa mwaka ujao wakati ambapo DA kinataraji kunufaika na rekodi mbovu ya kiuchumi ya serikali na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira.
Lakini chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters – EFF pia kinaonekana kuimarika, kikitafuta kura kutoka kwa Waafrika Kusini weusi wa tabaka la wafanya kazi ambao wanakasirishwa na ukosefu wa maendeleo chini ya utawala wa ANC. Katika hotuba yake ya kama kiongozi wa DA, Zille, mwenye umri wa miaka 64 alisema kuchaguliwa kwa kiongozi mpya wa chama kutakuwa ni “mwanzo mpya, siyo tu kwa chama hicho bali pia kwa Afrika Kusini”.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga