1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Angola wawasilisha shauri kupinga matokeo ya urais

Daniel Gakuba
2 Septemba 2022

Chama kikuu cha upinzani nchini Angola, UNITA kimewasilisha malalamiko kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita nchini humo. Matokeo hayo yalikipa ushindi wa kiwango cha chini chama tawala cha MPLA.

 UNITA leader speaks to journalists
Picha: António Cascais/DW

 

''Pingamizi dhidi ya matokeo rasmi limefikishwa katika tume ya taifa ya uchaguzi leo,'' alisema Faustino Mumbika, katibu mkuu wa chama cha UNITA akizungumza na shirika la habari la AFP.

Uchaguzi wa Agosti 24 nchini Angola ulikuwa wenye ushindani mkali nchini Angola, tangu nchi hiyo ilipoanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Soma zaidi: Angola: MPLA yatangazwa mshindi, UNITA yakataa matokeo

Matokeo yalitangaza Jumatatu wiki hii yakikipa chama cha MPLA asilimia 51.17 ya kura, na kumhakikishia kiongozi wa chama hicho, Joao Lourenco ambaye pia ni rais wa Angola, muhula wa pili madarakani.

Chama cha UNITA kilipata asilimia 43.95, hatua kubwa mbele ikilinganishwa na asilimia 26.67 kilichopata katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Rais wa Angola Joao Lourenco, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha MPLAPicha: Stringer/REUTERS

Aapa kuhakikisha kila kura inaheshimiwa

Lakini katika hotuba yake kwa njia ya video, mwenyekiti wa chama hicho ambacho zamani kilikuwa vuguvugu la uasi, Adalberto Costa Junior, alirudia msimamo wake kuwa UNITA haiyatambui matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

''Tutafanya kila kitu kuhakikisha kwamba kila kura imezingatiwa na kuheshimiwa,'' amesema Costa Junior.

Soma zaidi: Waangola kuamua kati ya Lourenco na Costa Junior

Kwa miaka mingi chama cha MPLA kimekuwa na ushawishi mkubwa juu ya mfumo wa uchaguzi, na asasi za kiraia zimekuwa zikihofia kuwa kinaingilia katika kupangilia matokeo.

Kati ya makamishna 16 wa tume ya taifa ya uchaguzi, wanne hawakusaini hati ya matokeo ya mwisho, wakielezea mashaka juu ya jinsi ulivyoendeshwa..

Chama cha UNITA kinapinga matokeo kwa msingi wa kwamba kulikuwapo mkanganyiko katika zoezi la kukusanya na kuhesabu kura.

Malalamiko kwenye tume ya uchaguzi ni hatua ya kwanza katika mchakato ambao unaweza kuchukua muda wa zaidi ya wiki moja.

Uchaguzi wa Angola wa mwaka huu ulikuwa na ushindani mkali baina ya MPLA na UNITAPicha: Sergio Picarra

Mahakama ya katiba yatarajia kupokea malalamiko

Mapema Alhamisi, msemaji wa Mahakama ya Juu ya Angola, Artur Torres, alieleza kuwa baada ya tume ya uchaguzi kufanya maamuzi yake, malalamiko yanaweza kupelekwa mahakamani.

Katika hotuba yake kwa njia ya vidio, mkuu wa UNITA, Costa Junior alisema matarajio yake ni kuwa taasisi hizo mbili; tume ya taifa ya uchaguzi na mahakama ya katiba ''zitafanya kwa ukweli majukumu yao.''

Soma zaidi: Ushindani mkali watarajiwa katika uchaguzi wa Angola

''Tumekuwa na amani kwa muda wa miaka 20, na tunahitaji kukumbatia kikamilifu mfumo wa kidemokrasia na utawala wa sheria,'' amesema.

Chama cha MPLA kimekuwa madarakani tangu Angola ilipopata uhuru wake kutoka Ureno mwaka 1975. Lakini ushawishi wa chama hicho umeporomoka katika uchaguzi wa mwaka huu, ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017 kilipojishindia asilimia 61 ya kura.

Uitikiaji ulikuwa kiwango cha chini cha asilimia 45 ya wapigakura wote waliojiandikisha.

 

-afpe,rtre, (str/ub/har/lb)

 

  

    

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW