1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani DRC wamuonya Rais Tshisekedi

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.26 Oktoba 2020

Muungano wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Lamuka, umemuonya Rais Felix Tshisekedi asidai kutatua shida zinazoikumba nchi, ukisema yeye pia ni miongoni mwa matatizo.

DR Kongo Präsident Félix Tshisekedi
Picha: République Démocratique du Congo/Presse Présidentielle

Hayo yamejiri baada ya hotuba Rais Tshisekedi aliyoutowa Ijumaa iliyopita, akitangaza kwamba ataanza wiki hii kukutana na viongozi wa kisiasa pia wale wa kijamii kwa lengo la kuunda muungano wa taifa ili kuweka mfumo mpya wa serikali. Kwa upande mwingine, mashirika ya kiraia yameipongeza hatua hiyo ya Rais Tshisekedi. 

Hotuba yake Rais Felix Tshisekedi ilikuwa imesubiriwa sana, kwani raia wa Congo walikuwa wakingojea maamuzi ya kutatua shida zinazoiandama serikali kwa wakti huu.

Soma pia: Mpasuko mkubwa muungano wa Tshisekedi, Kabila Congo

Matatizo hayo yanatokana na kutoelewana baina ya washiriki katika uongozaji wa nchi hii, yaani vyama vinavyomuunga mkono Rais Tshisekedi maarufu CACH, na vile vinavyomuunga mkono rais mstaafu Joseph Kabila, maarufu FCC.

Pendekezo lake Tshisekedi kukutana na viongozi wa kisiasa na wale wa kijamii limepokelewa vyema na muungano wa kanisa la kiprotestanti, ECC, pia mashirika ya kiraia yanaafiki hatua hiyo kuwa itasaidia kuunda serikali yenye maelewano kwa faida ya wakongomani.

"Ni fursa ya kurekebisha mambo kwani muungano FCC -CACH ulikuwa tatizo kwa Kongo. Tulihitaji watatuwe shida zetu, ila wao wenyewe waligeuka na kuwa matatizo. Halafu tunawaza mazungumzo hayo yatamsaidia rais." Amesema Jonas Tshiombela ambaye ni moja wa viongozi wa shirika la raia.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila (aliyevalia miwani ya jua) wakati wa kuapishwa kwa mrithi wake Rais Tshisekedi Januari 24, 2019.Picha: picture-alliance/AP/J. Delay

Lakini upande wake muungano wa upinzani Lamuka unaoongozwa na Martin Fayulu umepinga mpango huo wa Rais Tshisekedi, ukisema bado kiongozi huyo hajaelewa kwamba yeye ni miongoni mwa matatizo yanayoikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma pia: Rais Tshisekedi akutana na mtangulizi wake kujadili mivutano

Lamuka imesema ni vigumu kwa Tshisekedi kudai kwamba anaweza kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazoikabili nchi na kuongeza kuwa tatizo kubwa ni kwamba Kongo inaongozwa na taasisi zisizo halali, kwa hivyo Lamuka haitajihusisha na mambo ya kuzihalalisha taasisi hizo.

Kwa mjibu wake Prince Epenge, ambaye ni moja wa wasemaji wa Lamuka, muungano huo upo tayari kuyazungumzia mageuzi kuhusu taasisi. 

"Tatizo la kweli ni baina ya Kabila, Felix na raia kuhusu uhalali. Tunaweza tukazungumzie mageuzi kuhusu taasisi, ila katika mazingira yasiyotegemea upande wowote, ili kuambiana ukweli na hivyo, kutatua shida ya uhalali inayoikumba nchi." Amesema Prince Epenge.

Muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais mstaafu Joseph Kabila bado haujatoa tamko lolote kuhusu pendekezo la Rais Tshisekedi, ingawa muungano huo unatumaini kwamba hatua hiyo haitabadili wingi wake bungeni.

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW