Upinzani Guinea waitisha maandamano mapya
8 Oktoba 2019Muungano wa vyama vya upinzani nchini Guinea umeitisha maandamano kuanzia Oktoba 14 licha ya ukandamizaji unaofanywa na serikali kuyavunja maandamano baada ya Rais Alpha Conde kuzusha uvumi kuwa anataka kuwania muhula wa tatu wenye utata.
Mwezi uliopita, Conde mwenye umri wa miaka 81, aliwataka wananchi kujiandaa kwa kura ya maoni na uchaguzi, na hivyo kuzusha gumzo kuwa anapanga kupuuza zuio la kikatiba la kuwania kwa muhula wa tatu.
Conde ni kiongozi wa zamani wa upinzani ambaye aliingia madarakani 2010, na kuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Guinea.
Muungano wa upinzani wa National Front for the Defence of the Constitution - FNDC unapinga uwezekano wa kuwepo muhula wa tatu.
Muhula wa pili wa Conde ambao ndio wa mwisho chini ya katiba ya sasa, unakamilika Oktoba 2020.