1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Kenya kurudi barabarani dhidi ya IEBC

9 Desemba 2016

Ikiwa imesalia miezi minane tu kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, upinzani unatishia kufanya tena maandamano dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ukidai kukiukwa kwa utaratibu wa matayarisho ya uchaguzi huo.

Protest in Kenia Raila Odinga 07.07.2014
Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Muungano wa upinzani CORD unaoongozwa na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic Movement na kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetangula, unadai kwamba IEBC inapanga njema ya kuiba kura.

"Ukweli wa mambo ni kwamba mikakati tayari inawekwa ya kuiba kura kabla makamishna wapya hawajaingia. IEBC imefanya ukaguzi wa daftari la sajili wa wapiga kura kiholela bila kuzingatia kuondoa majina ya wapiga kura waliofariki, wale walio na umri wa chin nai wale waliojisajili mara mbili na kuhakikisha sajili hiyo ni safi," Musyoka aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa na upinzani kuwa ni njama za wizi ni lile la kuendelea kuhudumu kwa kwa makamisha wa zamani wa tume hiyo, ambao walitakiwa wawe wameshaondoka kufikia mwanzoni mwa mwezi Disemba.

"Makashina wa tume iliyovunjwa ambao wanatakiwa wawe wameenda nyumbani wanasisitiza waendelee kuwa ofisini ili wasimamie ununuzi wa vifaa vya uchaguzi kwa sababu ya fedha ambazo wanataka walipwe, lakini wacha niseme kwamba hakuwezi kuwa na tume bila makamishna," alidai Odinga.

Hata hivyo, IEBC yenyewe inasema kwamba haina lengo la kuwabakisha makamishna hao pale muda wa wengine watakapoingia. Mkurungenzi wa Tume hiyo, Ezra Chiloba, alijitetea kwa kusema kuwa makamishna hao, hata kama wapo, sio wenye dhamana ya utendaji wa siku kwa siku ndani ya IEBC.
 
"Makamishna hawakagui tenda, makamishna hawatangazi tenda na hawaidhinishi wala kutia saini tenda," alisema Chiloba.

Makamishna wakongwe wangalipo

Hadi sasa, bado makamisha wa zamani hawajaondoka ofisini licha ya tarehe ya mwisho kwa makamishna wapya kuingia ofisini kupita. 

Muungano wa upinzani ulifanya maandamano kwa muda wa miezi miwili mfululizo kati ya mwezi Mei na Juni kupinga utendaji kazi wa makamishna hao, hatua ambayo iliwalazimisha kujiuzulu.

Hata hivyo, sasa upinzani una wasiwasi kwamba muda uliosalia ni mdogo mno kwa IEBC kufanya matayarisho ya kuaminika, lakini Tume hiyo inasema kuwa inao uwezo wa kukamilisha kila kitu kwa wakati muafaka.

Mwezi Mei na Juni, upinzani ulifanya maandamano makubwa kupinga Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

"Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwani kila kitu kiko shwari. Tumetoa ratiba ya mpangilio wa mambo yatakavyoenda katika muda wa miezi minane," allisema Chiloba.

Leo (Disemba 9) ni siku ya mwisho kwa wagombea wa nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi ujao kujisajili katika ofisi za Tume ya Uchaguzi, huku changamoto ikiwa wagombea hawajajua watasimama kwa chama kipi, kwani hata uteuzi wa vyama haujafanyika.

 
Huku hayo yakiendelea Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanazunguka pembe zote za nchini wakizindua miradi ya maendeleo hasa ya ujenzi wa miundombinu hatua ambayo inaonekana kuwa kampeni za uchaguzi mkuu ujao, huku upinzani ukizidi kuikosoa serikali kutokana na kashfa za ufisadi, upendeleo na wizi wa mali ya umma.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW