1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Upinzani Korea Kusini wawasilisha mswada kumuondoa rais Yoon

4 Desemba 2024

Wabunge nchini Korea Kusini wamewasilisha mswada wa kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol baada ya kutangaza sheria ya kijeshi kabla ya kuibatilisha saa chache baadae. Hatua hiyo imezusha mogogoro wa kisiasa.

Maandamano Korea Kusini
Waandamanaji mjini Seoul walibeba mabango wakimtaka Rais Yoon akamatwePicha: Lee Jin-man/AP/dpa/picture alliance

Tangazo la kushtukiza la sheria ya kijeshi siku ya Jumanne lilisababisha mzozo na bunge, ambalo lilikataa jaribio lake la kupiga marufuku shughuli za kisiasa na kuvidhibiti vyombo vya habari, huku wanajeshi waliokuwa na silaha wakiingia kwenye jengo la Bunge la Kitaifa mjini Seoul.

Soma pia: Rais wa Korea Kusini akirii 'mapungufu' katika hotuba yake ya nadra

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Party (DP) kilimtaka Yoon, ambaye amekuwa madarakani tangu 2022, kujiuzulu au kukabiliwa na mashtaka. Lee Jae-myung ni kiongozi wa chama cha DP. "Kama wananchi wasingelizingira Bunge, lingevamiwa na askari wa vikosi vya nchi, ambao walivunja madirisha na wakapanda juu kujaribu kuingia. Shukrani kwa wananchi ambao walihatarisha maisha yao, kuwa tayari kupigwa risasi, kwa sababu walizuia wabunge kukamatwa, na chumba kikuu hakikukamatwa. Hii iliruhusu utatuzi wa kisheria wa kuivunja sheria ya kijeshi."

Upinzani wawasilisha mswada wa kumshtaki Yoon

Vyama sita vya upinzani vya Korea Kusini baadaye viliwasilisha mswada bungeni wa kumshtaki Yoon, huku upigaji kura ukipangwa kufanyika Ijumaa au Jumamosi.

Matukio ya fujo yalizuka huku wanajeshi wakijaribu kuliteka jengo la bunge nao waandamanaji wakipambana na polisiPicha: Cho Da-un/Yonhap/AP/picture alliance

Kulikuwa na mgawanyiko mkubwa katika chama tawala cha Yoon cha People Power pia, huku kiongozi wake akitaka Waziri wa Ulinzi Kim Yong-hyun afukuzwe kazi na baraza zima la mawaziri kujiuzulu.

Soma pia: Korea Kusini tayari kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini

Yoon aliliambia taifa katika hotuba yake ya televisheni jana jioni kwamba sheria ya kijeshi inahitajika ili kulinda nchi dhidi ya makundi yanayoiunga mkono Korea Kaskazini katika vita vyake dhidi ya serikali, na kulinda utaratibu huru wa kikatiba, ingawa hakutaja vitisho maalum.

Matukio ya fujo yalizuka huku wanajeshi wakijaribu kuliteka jengo la bunge nao waandamanaji wakipambana na polisi. Jeshi lilisema shughuli za bunge na za vyama vya kisiasa zitapigwa marufuku, na kwamba vyombo vya habari na wachapishaji watakuwa chini ya udhibiti wa amri ya sheria ya kijeshi.

Soma pia: Rais wa Korea Kusini akabiliwa na mtihani mgumu uchaguzi wa bunge

Lakini wabunge walikaidi vizuizi vya usalama na ndani ya saa chache baada ya tamko hilo, bunge la Korea Kusini, likiwa na wabunge 190 kati ya 300 waliohudhuria, likapitisha kwa kauli moja hoja ya kutaka sheria ya kijeshi iondolewe, huku wajumbe 18 wa chama cha Yoon wakihudhuria.

Yoon aliliambia taifa sheria ya kijeshi inahitajika ili kulinda nchi dhidi ya makundi yanayoiunga mkono Korea KaskaziniPicha: South Korea Presidential Office/AP/dpa/picture alliance

Marekani na NATO wazungumza

Rais kisha aliibatilisha sheria hiyo ya kijeshi, masaa sita tu baada ya kuitangaza. Waandamanaji nje ya bunge waliimba na kushangilia wakisema kuwa wameshinda.

Maandamano zaidi yalitarajiwa leo huku chama kikubwa cha wafanyakazi nchini humo, Korean Confederation of Trade Unions, kikipanga kufanya maandamano makubwa mjini Seoul na kuapa kufanya mgomo mpaka Yoon atakapojiuzulu.

Ikiwa Yoon atajiuzulu au kuondolewa madarakani, Waziri Mkuu Han Duck-soo atachukua nafasi hiyo hadi uchaguzi mpya utakapofanyika ndani ya siku 60.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema ameukaribisha uamuzi wa Yoon kulibatilisha tamko la sheria ya kijeshi.

Naye katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte amesema muungano huo wa kijeshi unafuatilia hali nchini Korea Kusini, lakini akaongeza kuwa uhusiano wake na Soeul ni imara.

Reuters, afp, dpa, ap

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW