1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Mali wasema utafanya kazi na wanajeshi

Sekione Kitojo
20 Agosti 2020

Muungano wa upinzani Mali umepuuzia juhudi zinazofanywa na mataifa ya kanda  hiyo kuzuwia mabadiliko ya serikali yanayoongozwa na wanajeshi waliofanya mapinduzi, ukisema utafanyakazi pamoja na viongozi hao wa mapinduzi

Mali Kati PK Putsch Anführer Ismael Wague
Picha: Getty Images/AFP/A. Risemberg

Jumuiya ya Kiuchumi ya mataifa ya  Afrika  magharibi ECOWAS, ambayo inakutana kujadili  mzozo  huo, imesimamisha  uanachama wa  Mali, kufunga  mipaka  na  kuzuwia  uingiaji  wa  fedha  katika nchi  hiyo  katika  hatua  ya  kujibu  uasi  uliotokea  siku  ya Jumanne  uliosababisha   mapinduzi dhidi  ya  serikali  ya  rais Ibrahim Boubacar Keita.

Kiongozi wa mapinduzi nchini Mali Assimi GoitaPicha: Getty Images/AFP/M. Konate

Muungano  unaofahamika  kama  M5-RFP  kundi  la  upinzani lililokuwa  linapinga  utawala  wa  Keita limesema  linafanyakazi pamoja  na  wanajeshi  waliofanya  uasi, na  kuviita  vikwazo vilivyowekwa  na   jumuiya  ya  ECOWAS  kuwa  ni  uchukuaji  wa hatua bila  kufikiria inayotokana  na  hofu ya baadhi  ya  viongozi  wa kikanda  kuwa  mapinduzi yaliyofanyika  yanaweza  kuanzisha machafuko  ya  kisiasa  katika  nchi  zao  pia.

"Viongozi  hao wanachukua  msukumo  kuiweka  ECOWAS dhidi ya Mali," amesema  msemaji  wa  kundi  hilo  la  M5-RFP Nouhoum Togo.

"M5-RFP  na  CNSP  ikiwa  na  maana  kamati ya taifa  ya uokozi wa  umma,  kwa  hivi sasa zinafanyakazi kwa  pamoja. Togo  alisema benki zitafunguliwa  na  kufanyakazi kama  kawaida leo Alhamis.Msemaji wa kamati ya mikakati ya M5-RFP Issa Kaou Djim amesema kila mtu atajumuishwa katika mchakato wa uongozi, wote ni  watu wa Mali.

Wanjeshi wa Mali wakilinda doria mjini Bamako baada ya mapinduzi Picha: Reuters/M. Kalapo

Hali ya maisha yaanza kurejea kawaida

Mji mkuu  Bamako ulikuwa  tulivu kwa  siku  ya  pili  mfululizo, siku moja  baada  ya  shirika  la  habari la  Reuters  kusema, wakati watu wanaonekana  kufuata miito ya msemaji wa  uongozi  wa  jeshi kanali Ismael Wague  wa kurejea  kazini na  kuendelea  na  maisha kama  kawaida.

Mapinduzi hayo, ambayo yameitikisa  nchi  hiyo  ambayo  tangu hapo inakumbwa  na  mapigano  ya  makundi ya  jihadi  pamoja  na machafuko  ya  umma, yamekumbana  na  shutuma  kali  kutoka jumuiya  ya  kimataifa.

Mapinduzi  pia  yamechochea  wasi wasi  kwamba  yanaweza kuvuruga  kampeni  za  kijeshi dhidi  ya wapiganaji  wa  jihadi   wenye mafungamano  na  kundi  la  al-Qaeda  na  kundi  linalojiita  Dola  la Kiislamu  yanayofanyakazi  zao  upande  wa  kaskazini na  kati nchini  Mali  na  eneo  kubwa  la  Afrika  magharibi  la  eneo  la Sahel.

Wanajeshi wa Ujerumani wakilinda eneo la kaskazini mwa Mali dhidi ya wapiganaji wa jihadiPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wakuu  wa  mataifa  15  wanachama  wa  ECOWAS wanatarajiwa kujadili mapinduzi  hayo  katika  kikao  kwa  njia  ya  vidio leo Alhamis.

Mwezi Julai , ujumbe kutoka  kundi  hilo  la  mataifa  ulishindwa kupata  makubaliano kati  ya  Keita na  upinzani, ambao umeendesha maandamano  makubwa  dhidi ya  serikali  katika  miezi ya  hivi karibuni.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW