Upinzani Misri wataka uchunguzi ufanyike
24 Desemba 2012Muungano wa upinzani wa Misri ujulikanao kama National Salvation Front umeitaka Tume ya Uchaguzi kuchunguza madai yao ya kuwepo kwa udanganyifu na ukiukaji wa sheria kwenye awamu zote mbili za mchakato huo uliomalizika mwishoni mwa juma lililopita.
Mmoja wa wajumbe wa muungano huo, Amr Hamzawy, amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Misri, Cairo kwamba wanataka tume ya uchaguzi ichunguze kwanza madai hayo kabla ya kuyatangaza rasmi matokeo ya kura hiyo.
Katika tamko lililotolewa kwenye mkutanao huo na waandishi wahabari, wapinzani hao wamesema kuwa kura ya maoni siyo mwisho wa njia bali ni sehemu tu ya mapambano na kwamba wataendelea kuwapigania raia wa Misri.
Pamoja na madai ya ukiukaji wa sheria kwenye kura ya maoni, upinzani unahoji pia juu ya uhalali wa kura hiyo kutokana na idadi ndogo ya watu waliojitokeza kushiriki mchakato huo. Ni asilimia 32 tu ya watu waliojiandikisha kupiga kura ndio walijitokeza vituoni kushiriki zoezi hlo.
Wapinzani kupinga matokeo mahakamani
Awali, wapinzani walishatangaza kuwa watayapinga matokeo ya kura hiyo ambayo taarifa zisizo rasmi zinaarifu kuwa imekubalika zaidi ya asilimia hamsini. Kituo cha televisheni cha taifa nchini Misri kimetangaza kuwa matokeo ya awali yanaonyesha ushindi wa asilimia 63 wa kukubalika kwa kura hiyo.
Chama cha Udugu wa Kiislamu cha Rais Mohammed Mursi kimeyakaribisha matokeo hayo na kuwataka wapinzani kuheshimu maamuzi ya umma. Matokeo rasmi huenda yakatangazwa baadae hii leo.
Kufuatia vuta-nikuvute hiyo, Ujerumani imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru na wa wazi juu ya matokeo hayo. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema: "Katiba inaweza kukubaliwa ikiwa tu mchakato wa kuipitisha umefanyika kwa uwazi".
Westerwelle ameongeza kuwa si matumizi ya nguvu mitaani yatakayoionyesha Misri njia ya kuchukua, bali ni hisia za maelewano na uvumilivu ndizo zitatoa majibu ya mustakabali wa baadae wa nchi hiyo.
Matokeo rasmi bado hayajatangazwa
Hata hivyo Afisa wa Tume ya iliyoendesha zoezi hilo bwana Mohamed el-Tanobly ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hakuna tarehe maalumu iliyopangwa kwa ajili ya kutolewa matokeo ya mwisho ya kura hiyo. Hapo awali Shirika la Habari la Misri (MENA) lilitangaza kuwa matokeo rasmi yangetolewa leo Jumatatu.
Rais Mohammed Mursi na Chama chake cha Udugu wa Kilslamu wanaunga mkono mswada huo wakisema kuwa ni muhimu kwa ajili ya kurejesha utulivu nchini humo baada ya vuguvugu la kumng'oa madarakani kiongozi wa zamani Hosni Mubarak mwaka uliopita.
Lakini wapinzani wanaiona rasimu hiyo ya katiba kama njia ya kuweka utawala wa Kiislamu na ukiukaji wa haki za binaadamu hasa haki za wanawake pamoja na kuudidimiza uhuru wa mahakama.
Kama mswada huo utapitishwa, Misri itakwenda katika uchaguzi wa bunge katika kipindi cha miezi miwili ijayo, kuwachagua wabunge watakaochukua nafasi ya bunge la sasa linalotawaliwa na wanachama wa Chama cha Udugu wa Kiislamu ambalo lilivunjwa na mahakama kabla ya uchaguzi wa Juni uliomleta madarakani Rais Mursi.
Masuala ya bunge nchini Misri kwa sasa yanasimamiwa na baraza la seneti ambalo pia lina wafuasi wengi wa Kiislamu.
Mwandishi: Stumai George/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba.