Upinzani nchini Ujerumani washinikiza uchaguzi wa mapema
7 Novemba 2024Ujerumani imeingia katika kipindi cha atiati ya kisiasa leo baada ya serikali yake ya muungano wa vyama vitatu kuvunjika usiku wa kuamkia leo, katika siku ambayo Donald Trump alishinda uchaguzi wa Marekani. Haya yamejiri kufuatia miezi kadhaa ya malumbano ya ndani kwa ndani kati ya vyama hivyo.
Katika kile kilichowashtua wengi, Kansela Olaf Scholz amemuachisha kazi waziri wake wa fedha, Christian Lindner wa chama cha Free Democrats, FDP, jambo lililokipelekea chama hicho kujitoa katika serikali hiyo ya muungano. Chama cha Social Democrats, SPD, na kile cha wanamazingira cha Kijani ndivyo vilivyosalia katika serikali iliyopoteza wingi wake bungeni.Vyama vya serikali ya muungano Ujerumani vyakutana kujaribu kutatua mgogoro
Scholz amesema kwamba ataitisha kura ya imani mnamo Januari 15 ili wabunge waamue iwapo wataitisha uchaguzi wa mapema, ambao utafanyika miezi sita kabla ya muda. Uchaguzi mkuu ulikuwa umepangiwa kufanyika Septemba mwakani.
Scholz amesema kwamba atawasiliana na kiongozi wa chama cha upinzani cha kihafidhina, Friedrich Merz, ambaye anaongoza katika tafiti za maoni, ili amsaidie kupitisha miswada muhimu kuhusiana na uchumi na ulinzi.