1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani nchini Zimbabwe, wanyakua nafasi ya Uspika.

Nyanza, Halima25 Agosti 2008

Upinzani nchini Zimbabwe leo umepata ushindi wa kihistoria, baada ya mgombea wa MDC kushinda nafasi ya Spika wa bunge hali ambayo inaipa chama hicho kudhibiti nafasi hiyo muhimu kwa mara ya kwanza.

Lovemore Moyo, kutoka chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change, akipungia mkono muda mfupi, baada ya kuchaguliwa kuongoza bunge.Picha: AP

Mwanachama huyo wa Chama Kikuu cha Upinzani cha MDC, Lovemore Moyo amepata kura 110, dhidi ya mpinzani wake Paul Themba Nyathi, aliyepata kura 98, ambaye alikuwa mpinzani pekee kutoka chama kilichojitenga na MDC, kinachoongozwa na Arthur Mutambara.

Chama tawala kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe, cha ZANU PF, hakikutoa mgombea wake ili kupambana na Bwana Moyo, badala yake kilimuunga mkono Bwana Nyathi kutoka chama kidogo cha MDC, kilichojitenga.

Chama cha MDC, kina wabunge wapatao 100, lakini wakati zoezi hilo la upigaji kura, likifanyika kulikuwa na wabunge 99, walioweza kupiga kura.

Chama cha upinzani kinachoongozwa na Arthur Mutambara kina wabunge 10, huku mbunge mmoja akiwa ni wa kujitegemea.

Bunge la nchi hiyo linawabunge wapatao 210.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, yaliyopokewa kwa shange kubwa na wabunge wa chama cha upinzani cha MDC, msemaji wa kiongozi wa chama hicho cha upinzani Morgan Tsangirai, George Sibotshiwe ameongeza kusema kuwa ushindi huo, unadhihirisha wazi kwamba MDC ni chama cha watu.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Bwana Moyo amesema atahakikisha kuwa sheria za kimaendeleo zinapitishwa na kwamba bunge hilo lisiwe sehemu ya kupitisha kila kitu kinachotakiwa na serikali.

Kufuatia matokeo hayo, maafisa wa chama Kikuu cha upinzani ambacho ndicho kilichopata ushindi, wamekadiria kuwa kura nne alizopata mgombea wao zimetoka kwa wabunge wa chama tawala cha ZANU PF, na nyingine zilitoka kwa chama cha upinzani kinachoongozwa na Bwana Mutambara.

Ushindi huo wa leo umeelezwa kwamba unaweza kuvuruga mipango ya Rais Mugabe ya kulishawishi bunge la nchi hiyo na kujaribu kuunda serikali bila ya Bwana Tsvangirai.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana ndani ya chama hicho cha MDC, kwa sasa chama hicho kinadhibiti bunge na kwamba kina nguvu ya kutoa maamuzi yoyote kuhusu bunge hilo.

Mapema leo kabla ya uchaguzi huo wa Spika kufanyika, wabunge wawili wa chama hicho cha MDC, walikamatwa na polisi wakati wakiingia kwenye eneo hilo la bunge kwa shughuli ya kuapishwa, hali ambayo chama hicho cha upinzani kilidai kuwa ni mpango wa kupunguza wingi wao bungeni wakati ambao walikuwa wakijiandaa na zoezi la kuchagua Spika mpya.

Hata hivyo wabunge hao, Shua Mudiwa na Eliah Jembere waliachiwa baadaye na kuweza kushiriki katika zoezi hilo la upigaji kura.

Wakati huohuo Chama tawala cha ZANU PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe kimeshinda uspika wa baraza la Seneta.

Mgombea wa ZANUPF, Edna Madzongwe amepata kura 58 dhidi ya 28 alizopigiwa mgombea wa upinzani.

Bado kumekuwa na mvutano katika mazungumzo ya kugawana madaraka kati ya Rais Mugabe na upinzani, ambapo MDC wanatoa wito kwa Bwana Tsvangirai kudhibiti serikali, huku ZANU PF wakisisitiza kuwa Rais Mugabe aendelee kubaki kama mkuu wa nchi na serikali.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW