1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Pakistan wamtaka Waziri Mkuu Sharif Ajiuzulu

11 Julai 2017

Familia ya Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif pamoja na wandani wake wameipinga ripoti moja ya mahakama iliyokuwa inachunguza mali ya waziri huyo mkuu.

Bosnien-Herzegowina Pakistans Premierminister Nawaz Sharif
Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz SharifPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Emric

Familia hiyo imesema ripoti hiyo haina maana kwa kudai kwamba familia ya Sharif ina mali kushinda mapato yake. Wapinzani wa Waziri Mkuu huyo Jumanne walimtaka ajiuzulu baada ya ripoti hiyo kutolewa.

Jopo la  uchunguzi lililoundwa na Mahakama ya Juu nchini humo ili kufanya uchunguzi wa madai yaliyoibuka kufuatia ule ufichuzi wa makaratasi ya Panama yaliyoonesha mabwenyenye kuficha pesa zao katika mataifa ya Ulaya, lilifanya uchunguzi wake dhidi ya familia ya Sharif kwa kipindi cha miezi miwili na likawasilisha matokeo ya uchunguzi huo mbele ya mahakama Jumatatu.

Jopo hilo lilimuhoji Sharif mwenyewe, wanawe wawili wa kiume, mwanawe wa kike na watu wengine katika familia yake. Uchunguzi huo hatimaye uliafikia kwamba kuna tofauti kubwa baina ya pato la Waziri huyo Mkuu na vyanzo vyengine vyake vyengine vya mapato vinavyojulikana.

Chama cha Jamaat-e-Islami kimemtaka Sharif ajiuzulu

Huku ikiwa ripoti hiyo haikuwekwa wazi mara moja, kulikuwa na kurasa zilizopenyezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kiongozi wa upinzani Imran Khan akamtaka Sharif ajiuzulu kufuatia matokeo hayo, yaliyowatwisha  lawama wanawe mmoja wa kike na wawili wa kiume.

Mwanawe wa kike wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Maryam NawazPicha: Reuters/F. Mahmood

Chama cha mrengo wa kulia cha Jamaat-e-Islami pamoja na kundi la rais wa zamani Asif Ali Zardari pia, walimtaka Sharif ajiuzulu.

Ripoti hiyo inasema biashara za Sharif pekeyake, hazitoshi kuelezea mali ya familia yake, ambazo ni pamoja na nyumba katika mtaa mmoja wa kifahari mjini London. Kulingana na vyombo vya habari vya Pakistan, ripoti hiyo vile vile imependekeza shirika linalokabiliana na ufisadi nchini Pakistan, limfungulie mashtaka Sharif.

Mahakama ya Juu itaamua iwapo imfungulie Sharif Mashtaka

Washirika wake wa kisiasa lakini wameipinga ripoti hiyo wakiitaja kama njama dhidi ya Waziri mkuu huyo na demokrasia nchini Pakistan. Mshirika wa karibu wa Sharif ambaye pia ni waziri wa ulinzi wa Pakistan Asif Khawaja, alisema ripoti hiyo ina mapungufu chungunzima na chama tawala kitakata rufaa dhidi ya matokeo hayo katika Mahakama ya Juu.

Mahakama ya Juu ya PakistanPicha: Reuters/C. Firouz

Mahakama hiyo ya Juu sasa itaamua jinsi itakavyoshughulikia ripoti hiyo na iwapo ifungue mashtaka.

Sharif siku zote amekuwa akikanusha kufanya makosa yoyote katika madai ya kwamba familia yake imekuwa ikitumia kampuni zake zilizoko katika nchi za nje kununua nyumba za kifahari mjini London na anasema familia yake imepata mali yake kwa njia halali.

Kikosi hicho kilichofanya uchunguzi kilijumuisha wanachama kutoka mashirika ya kiraia na mashirika yenye nguvu ya kijeshi lakini uchunguzi huo uliingizwa siasa baada ya waungaji mkono wa Sharif na wapinzani wake kuzozana kuhusiana na uchunguzi uliokuwa ukifanywa na shirika hilo na upande waliokuwa wanaegemea wanachama wake.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu