1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Upinzani Pakistan wasema kukamatwa kwa Khan kutazusha balaa

22 Agosti 2022

Viongozi wa upinzani nchini Pakistan wameonya kwamba endapo waziri mkuu wa zamani, Imran Khan, atakamatwa, mstari mwekundu utakuwa umevuukwa, huku polisi ikifunguwa mashitaka yanayohusiana na ugaidi dhidi yake.

Pakistan | Imran Khan | ehemaliger Premierminister
Picha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Mamia ya watu walikusanyika nje ya nyumba yake asubuhi ya leo Jumatatu, wakikusudia kuwazuwia polisi kumkamata, ingawa waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa akipambana na kesi kadhaa zilizofunguliwa na serikali dhidi yake kwa kipindi kirefu bila ya kuwekwa kizuizini.

Waziri wa zamani wa habari, Fawad Chaudhry, alituma ujumbe kupitia mtandao wa Twitter uliosomeka kwamba: "Popote ulipo, elekea Bani Gala leo na onesha mshikamano wako naImran Khan. Imran Khan ni mstari usiopaswa kuvuukwa kwetu." Bani Gala ndipo nyumbani kwa Khan. 

Habari zinasema kuwa kile kiitwacho Ripoti ya Taarifa ya Awali ilifunguliwa na polisi hapo jana Jumapili - ikiwa ni hatua ya kwanza ya mchakato ambao unaweza kupelekea mashitaka rasmi na kukamatwa kwa mcheza kriketi huyo wa kimataifa aliyegeuka mwanasiasa mkubwa nchini mwake. 

Hata hivyo, wanasheria wake walikimbia haraka mahakamani kuomba dhamana ya kabla ya kukamatwa, ambayo walipewa na itakayodumu angalau hadi kesho Jumanne.

Mpaka majira ya mchana, bado kulikuwa na idadi ndogo ya polisi nje ya makaazi ya Khan, huku wafuasi wake wapatao 500 wakikusanyika kwenye kiunga hicho cha Bani Gala.

Wafuasi wajitolea kumlinda

Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan, Shehbaz Sharif.Picha: Asif Hassan/AFP/Getty Images

Mmoja wa wafuasi hao, Muhammad Ayub, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba alisafiri usiku mzima kutoka Peshawar kuja kumuunga mkono Khan na kwamba yeye na wenzake wangeliandama na kuziba njia zote endapo kiongozi huyo angelikamatwa. 

Taarifa kutoka chama cha Khan, Tahreek-e-Insaf, imesema kuwa tuhuma hizi ni za uzushi, ikiilaumu kwa kuandaa mazingira ya kuitumbukiza nchi kwenye machafuko makubwa.

Siku ya Jumamosi, Khan alimkosoa hakimu mmoja wa mahakama ya mwanzo kwa kuamuru afisa wa chama chake kuwekwa kizuizini, ambaye pia chama chake inasema aliteswa vibaya akiwa mikononi mwa vyombo vya dola. 

Tangu ang'olewe madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni mnamo mwezi Aprili mwaka huu, Khan amekuwa akiendesha mikutano na maandamano makubwa nchi nzima, akizionya taasisi za dola, likiwemo jeshi, kutokuiunga mkono serikali ya mseto inayoongozwa na hasimu wake wa muda mrefu wa kisiasa, Shehbaz Sharif. 

Lengo kuu la Khan ni uchaguzi mkuu wa mapema, kabla ya ule wa kawaida ambao ulitakiwa kufanyika kabla ya Oktoba mwakani, lakini serikali haionekani kuwa na dalili yoyote ile ya kuingia kwenye uchaguzi, ikidai kupambana na hali ngumu ya kiuchumi kwa sasa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW