Upinzani Serbia wapinga matokeo ya uchaguzi kwa vurumai
25 Desemba 2023Maafisa wa usalama walitumia gesi ya kutoa machozi kuwadhibiti waandamanaji waliokuwa wakitumia mawe na milingoti ya bendera kupasua vioo vya majengo hayo ya utawala. Wafuasi hao wa upinzani wanalalamika kuhusu tuhuma za wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa uliofanyika Disemba 17.
Matokeo ya uchaguzi huo yanaonesha chama cha rais Aleksandar Vucic wa nchi hiyo cha Serbia Progressive kimenyakua ushindi wa viti vingi vya bunge la taifa pamoja na serikali za miji ikiwemo mji mkuu, Belgrade. Upinzani unasema umeporwa ushindi kwenye matokeo ya uchaguzi wa mji mkuu.
Rais Vucic ameyataja maandamano ya leo usiku kuwa jaribio la kuipindua serikali na ni njama kutoka mataifa ya kigeni. Hata hivyo kiongozi huyo hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai hayo.