1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan Kusini

Upinzani Sudan Kusini wapinga mashtaka dhidi ya Machar

12 Septemba 2025

Upinzani nchini Sudan Kusini umekosoa vikali mashtaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu yanayomkabili Makamu wa Rais Riek Machar, wakiyataja kama ya kisiasa na yenye lengo la kumdhibiti kisiasa.

Juba | Sudan Kusini | Riek Machar
Makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Upinzani nchini Sudan Kusini umepinga vikali hatua ya kushtakiwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar kwa makosa ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu. Reath Muoch Tang, afisa mkuu katika chama cha Machar amesema mashtaka hayo yamebuniwa ili serikali iweze kuyafuta makubaliano ya kugawana madaraka.

Waziri wa sheria wa Sudan Kusini Joseph Geng Akech amesema makamu huyo wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amefunguliwa mashtaka hayo kutokana na shambulio lililofanywa na wanamgambo wa kikabila kwenye kambi ya kijeshi katika kaunti ya Nasir kwenye jimbo la Upper Nile kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini ambako zaidi ya wanajeshi 250 waliuawa.

Waziri wa sheria Joseph Geng Akech amesema kesi inayomkabili Riek Machar inaonyesha wazi kwamba serikali haitasita kuwawajibisha wanaotenda maovu dhidi ya jeshi na raia wa Sudan Kusini hata kama wana vyeo na ushawishi wa kisiasa.

Washirika wa Machar pia wameshtakiwa, huku baadhi wakiwa kizuizini

"Ushahidi zaidi unaonyesha kuwa kundi la White Army liliendesha shughuli zake kwa kuamriwa na  viongozi fulani wa SPLM-IO akiwemo Dr. Riek Machar kupitia miundo iliyopangiliwa ya kijeshi na kisiasa. Wahusika wakuu ni wanane na mashtaka yalifunguliwa kwa mujibu wa sheria za Sudan Kusini na zile za kimataifa. Mashtaka hayo ni ya mauaji, kula njama za kuipindua serikali na mengine yanayohusiana na ugaidi na kufadhili ugaidi," ameeleza Akech.

Serikali imesema Machar na watu wengine 20 wanawajibika na uvamizi uliofanywa na kundi la watu wa kabila la Nuer maarufu kama White Army ambalo ni kabila la Riek Machar mapema mwezi Machi mwaka huu, ambapo wakati wa uvamizi huo mali za watu pia ziliharibiwa.

Makubaliano tete ya kugawana madaraka kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza Machar yameingia doa kwa miezi kadhaa katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Kurejea kwa Riek Machar Sudan Kusini

00:52

This browser does not support the video element.

Makubaliano hayo yalivurugika zaidi siku ya Alhamisi baada ya Machar aliyekuwa anazuiliwa nyumbani kwake, kushtakiwa kwa makosa ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu ambapo hii leo ameshitakiwa rasmi.

Mashitaka dhidi ya Riek Machar yanazidisha uhasama kati ya kambi mbili kuu za kisiasa nchini Sudan Kusini ambazo ni kambi inayoongozwa na Rais Salva Kiir na ile ya Machar ambazo ziliingia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2013 hadi mwaka 2018 ambapo takriban watu 400,000 waliuawa.

Mataifa yenye nguvu duniani yamekuwa yakitoa wito mara kwa mara wa kuachiliwa huru Makamu wa Rais Riek Machar na yamekuwa yakitahadharisha kwamba kuzuiliwa kwake kunaweza kuirejesha Sudan Kusini katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vyanzo: AFP/RTRE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW