Upinzani Syria warejesha udhibiti mji muhimu wa Idlib
27 Februari 2020Wapiganaji wa upande wa upinzani nchini Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wameweza leo kurejesha udhibiti wa mji muhimu wa Sarqeb wa kaskazini-magharibi mwa Syria ambao hivi karibu ulikamatwa na vikosi vya serikali ya Syria. Halikadhalika wamezuia barabara inayounganisha mji mkuu wa Damascas na mji wa kaskazini wa Aleppo.
Shirika la Kusimamai Haki za Binadamu Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema wapiganaji hao wa upande wa upinzani waliukamata mji huo kufuatia mashambulizi makali ya mabomu yaliyofanywa na wanajeshi wa Uturuki. Uturuki na Urusi zinaunga mkono pande mbili tofauti katika vita vya nchini Syria. Uturuki inayasaidia makundi ya upinzani huku Urusi ikiiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Hatua hiyo ya kurejesha udhibiti wa mji huo wa Sarqeb inavirejesha nyumba vikosi vya al-Assad. Ambavyo kupitia kampeni ya wiki kadhaa, vimekuwa vikipiga hatua kwa kukamata miji na vijiji tofauti vya mkoa wa Idlib, kwa msaada wa Urusi.
Maelfu wapoteza makazi Idlib
"Wanajeshi wetu wameweza kurejesha udhibiti wa miji na vijiji kadhaa katika siku chache zilizopita baada ya kuua idadi kubwa ya magaidi, kuzuia njia zao za kuingia na kutoka pamoja na kuharibu makao yao makuu," amesema msemaji wa jeshi la serikali Jenerali Ali Mayhoub.
Shirika hilo la kusimamia haki za binadamu Syria pia limethibitisha kwamba vikosi vya jeshi la serikali vimefanikiwa kuchukua udhibiti kamili wa eneo la kusini la mkoa wa Idlib, kufuatia mashambulizi yao dhidi ya waasi. Katika siku tatu zilizopita, vikosi hivyo vya serikali vimekamata takriban miji 60 pamoja na vijiji kusini mwa Idlib, eneo linalopakana na mkoa wa Hama.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Desemba yalipoanza mashambulizi hayo ya vikosi vya serikali watu wapatao 950,000 wamepoteza makazi yao, na wengine 300 wamepoteza maisha katika mkoa huo wa Idlib. Mapigano pia kati ya wanajeshi wa Syria na wa Uturuki yamesababisha vifo vya wanajeshi 18 wa Kituruki.
Vyanzo: (rtre,ap)