1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania waelezea figisu kuelekea uchaguzi

8 Novemba 2024

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimeilalamikia Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)nchini humo kuvihujumu baada ya majina ya wanachama wao waliochukua fomu kuwania nafasi za uongozi.

Msafara wa Chadema Arusha
Bendera na wafuasi wa Chadema TanzaniaPicha: Kelvin Emmanuel

Vyama vya upinzani vya Chadema, ACT – Wazalendo na CUF, vimelalamika kufanyiwa hujuma kwa wagombea wao ambao wameenguliwa katika orodha ya wanaowania uongozi wa serikali za mitaa, katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 27. Hata hivyo, vyama hivyo vimejinasibu kutosusia uchaguzi huo na badala yake vinakwenda kushiriki uchaguzi huo.

Wakati wapinzani wakilalamikia hujuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waweke pingamizi ndani ya siku 2 kuanzia leo Novemba 8 na kesho Novemba 9.

Uchaguzi wa ndani wa chama cha upinzani cha ACT-WazalendoPicha: Office of the First Vice President of Zanzibar

Mchengerwa ameongeza kuwa iwapo mgombea hatoridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi juu ya pingamizi lake, ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ndani ya muda usiozidi siku nne baada ya uamuzi huo kutolewa. Maana yake Rufaa ziwasilishwe kuanzia Oktoba 10 hadi  Novemba 13, 2024 kwa kamati ya Rufaa.

Soma: Tanzania yakamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura

Akizungumza na wanahabari leo Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje wa Chadema, amesema licha ya rafu hizo, chadema hakiko tayari kususia uchaguzi huo kama walivyofanya 2019.

Aidha, Mrema amesema chama chake kilisimamisha wagombea kwa asilimia 75 katika halmashauri zote nchini ambako hata hivyo asilimia 95  ya wagombea wao  wameenguliwa sababu zikiwa ni zile zinazojirudia, ikiwamo umri, uraia na kushindwa kujieleza.

Profesa Ibrahim Lipumba wa CUFPicha: Said Khamis/DW

Wakati Chadema wakiyasema hayo, chama cha ACT Wazalendo, wao kadhalika wamelalamika kuchezewa rafu baada ya wagombea wao wa nafasi za uongozi wa serikali za mitaa kuenguliwa wakidai, wameenguliwa bila sababu za msingi.

Msemaji wa Masuala ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, Rahma Mwita amesema idadi kubwa ya wagombea wa chama hicho wamekatwa bila sababu za msingi.

Soma kwa kina: HRW: Tanzania ishughulikie haki za binadamu kabla ya uchaguzi

Oktoba mwaka huu baadhi ya wanaharakati wa masuala ya siasa, walifungua kesi ya kupinga TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, ambayo hata hivyo mahakama iliamuru TAMISEMI kuendelea na usimamizi wa uchaguzi huo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa katika taifa hili la Afrika Mashariki unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na kwa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Novemba 27.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW