1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wakosoa taarifa ya Kabudi

George Njogopa27 Februari 2020

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimekosoa vikali taarifa iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo katika kikao cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva

Aussenminister Palamagamba Kabudi von Tansania
Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Waziri huyo alisema kwamba Tanzania inajivunia jinsi inavyoheshimu haki zote za binadamu. Akizungumza kwenye kikao hicho,hapo jana mjini Geneva Uswisi Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi alisemaTanzania inaheshimu na itaendelea kutekeleza kwa vitendo haki zote za binadamu bila ubaguzi na kwamba madai yanayoishutumu Tanzania kukiuka haki hizo ni propaganda tupu.

Waziri huyo alizitaja baadhi ya sheria ikiwamo ile inayohusu vyama vya siasa na huduma ya vyombo vya habari kuwa zimetungwa kwa kuzingatia maslahi ya makundi yote.

Hata hivyo, vyama vya upinzani vimekosoa taarifa hiyo vikidai vinapitia katika wakati mgumu. Vinasema, sheria ya vyama vya siasa iliyopitishwa mwaka jana, ni mojawapo ya vizingiti ambavyo vinabinya nafasi ya vyama hivyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano wa chama cha wananchi Cuf Mohammed Ngulangwa amesema ingawa kwa kiasi fulani kumekuwa na hatua za kupigiwa mfano lakini kwa ujumla wake, taarifa ya waziri Kabudi hajafahamisha ukweli jumla wa mambo ulivyo.

Wakosoa zuio la mikutano ya kisiasa

Nacho chama cha ACT Wazalendo kimetaja zuio la kufanya mikutano ya siasa pamoja msajili wa vyama vya siasa kuwa na mamlaka makubwa kama baadhi ya mambo yanayotia doa. Kaimu katibu wake, Doroth Semu anasema wakati huu ambapo taifa likielekea katika uchaguzi mkuu vyama vya upinzani bado vimeendelea kubanwa.

Mbali ya kutoa ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu katika kikao cha 43 Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea Geneva, Uswisi Waziri Kabudi pia aliutaja uchaguzi mkuu ujao akisema Tanzania imejiandaa kikamilifu.

Aliiambia jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi, huru na wa haki na kwamba Tanzania itaalika waangalizi wa kimataifa kushuhudia uchaguzi utakavyoendeshwa.

Mwandishi: George Njogopa/Dar es Salaam

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW