1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wataka Samia aapishwe mara moja kuwa Rais

Sylvia Mwehozi
18 Machi 2021

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Zitto Kabwe ametaka kuapishwa mara moja kwa makamu wa rais ili kuepuka ombwe la kikatiba baada ya wiki mbili za kutokuwa na uhakika wa mustabali wa uongozi wa nchi. 

Samia Suluhu
Picha: DW/E. Boniphace

Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan alilihutubia taifa Jumatano jioni kupitia televisheni wakati alipotangaza kifo cha rais Magufuli kutokana na maradhi ya moyo ambayo yalikuwa yakimsumbua kwa muda mrefu. Bi Samia Hassan  alisema mipango ya mazishi inaendelea kwa ajili ya kiongozi huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 61, lakini hakuasema chochote kuhusu muda wa kuapishwa kwake. Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe amelieleza shirika la habari la Reuters kuwa "makamu wa rais lazima aapishwe mara moja", akiongoza kuwa "katiba hairuhusu ombwe, mara tu inavyokuwa rasmi kuwa rais amekufa, hatua inayofuata inakuwa kwa makamu wa rais kuapishwa".

Makamu wa rais Samia na rais Magufuli enzi za uhai wakePicha: DW/Said Khamis

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, makamu wa rais Samia Suluhu Hassan mwenye umri wa miaka 61 anapaswa kuchukua madaraka ya urais kwa kipindi chote kilichobaki cha miaka mitano ambayo Magufuli alianza kukitumikia mwaka uliopita baada ya kushinda muhula wa pili. Atakuwa rais wa kwanza mwanamke katika taifa hilo la Afrika mashariki na wa kwanza katika ukanda mzima kushika madaraka ya juu.

Naye mpinzani mkuu wa Magufuli katika uchaguzi wa mwezi Oktoba Tundu Lissu, alisema ilikuwa ni wakati sasa kwa taifa kufungua ukurasa mpya akiongeza kwamba "miaka mitano ambayo Magufuli amekuwa rais amesababisha maafa katika nchi". Lissu aliyasema hayo Jumatano katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Kenya KTN News. "Magufuli amefariki kutokana na corona, hiyo ni moja, mbili Magufuli hajafa jioni hii, ninazo taarifa kimsingi kutoka chanzo ambacho kilinieleza alikuwa akiumwa vibaya sana. Ninazo taarifa kuwa Magufuli alifariki tangu Jumatano iliyopita".

Hatua ya Magufuli kutoonekana hadharani tangu Februari 27, ilizusha uvumi kwamba ameambukizwa COVID-19. Mnamo Machi 12, maafisa wa serikali walikana kuwa alikuwa mgonjwa na siku ya Jumatatu wiki hii makamu wa rais aliwataka  watanzania kupuuzia uvumi huo kutoka nje ya nchi akisema kwamba ilikuwa ni kawaida kwa mtu yeyote kukaguliwa mafua au homa. Watu kadhaa walikamatwa wiki hii kwa madai ya kueneza uvumi huo juu ya afya kiongozi katika mitandao ya kijamii.

Hayati rais Magufuli na makamu wake Samia wakati wa uchaguziPicha: DW/S. Khamis

Ingawa makamu wa rais Samia Suluhu amekuwa akitetea hadharani mtindo wa uongozi wa Magufuli na kumwakilisha mara nyingi nje ya nchi, lakini yeye huzungumza kwa upole zaidi, bila kupingana na amekuwa mwepesi kufanyiwa mahojiano na vyombo vya habari.

Katiba ya Tanzania inasemaje baada ya kifo cha Rais?Magufuli alikuwa akipuuza vikali ugonjwa wa  COVID-19 akiwahimiza watanzania kuachana na uvaaji barakoa na kuzikataa chanjo akieleza kuwa ni njama za mataifa ya magharibi na hivyo kulitia wasiwasi shirika la afya ulimwenguni WHO. Tanzania iliacha kutoa rasmi takwimu za ugonjwa wa corona mwezi mei mwaka jana ambapo wakati huo kulikuwa na visa 509 na vifo 21. Magufuli anakuwa rais wa kwanza kufikia madarakani nchini Tanzania.

Mapema leo asubuhi, hali katika mitaa ya Dar es salaam jiji la kibiashara ilionekana kuwa ya majonzi huku baadhi ya wakaazi wakisimama kwenye vibanda vya magazeti wakisoma vichwa vya habari na wengine wakitokwa na machozi. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema "Marekani imejizatiti kuendelea kuunga mkono watanzania wanapotetea kuheshimu haki za binadamu na misingi ya uhuru pamoja na kufanya kazi katika kupambana na COVID-19".

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW