Upinzani Togo kuandamana kupinga kuahirishwa uchaguzi
5 Aprili 2024Ikulu ya nchi hiyo ilitangaza siku ya Jumatano kwamba inausitisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike mnamo Aprili 20 bila hata hivyo kutangaza tarehe mpya.
Mivutano kati ya serikali ya rais Faure Gnassingbe na upinzani imefikia kiwango cha juu kabisa tangu bunge lilipoidhinisha mageuzi tata ya katiba ambayo wakosoaji wanasema yanalenga kumbakisha madarakani kiongozi huyo wa Togo.
Kwenye tangazo lao, vyama vinne vya upinzani na asasi moja ya kiraia wamewataka raia kumiminika mitaani kwa siku tatu za Aprili 11,12 na 13.
Wamesema wanataka kutuma ujumbe wa kupinga kile wamekitaja kuwa majaribio ya kuhalalisha "mapinduzi ya kikatiba" yanayofanywa na utawala wa Gnassingbe.
"Tunapinga vikali jaribio la utawala kutucheza shere, na jitihada zao za kutaka kuhalalisha mapindizi yake ya kikatiba," imesema sehemu ya taarifa yao.
Serikali yatoa sababu ya kuupiga kalenda uchaguzi wa Bunge
Yafaa kukumbusha hapa kuwa uchaguzi wa bunge la Togo ulikwishaahirishwa hapo kabla na upinzani unasema bunge la nchi hiyo linalotawala na chama cha rais Gnassingbe cha UNIR limepoteza mamlaka yake kisheria kutokana na kutofanyika kwa uchaguzi.
Waziri wa Utumishi wa Umma Gilbert Bawara alikiambia kituo kimoja cha redio kwamba mashauriano yanahitajika kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge. Amesema hilo litasaidia kuhakikisha uwazi hasa kuhusu mabadiliko ya katiba.
"Ninaamini itakuwa ni suala la msingi na kwa heshima ya wagombea, heshima kwa watu wa Togo na wapigakura, kwamba waelewe utaratibu ulivyo kabla ya kuingia kwenye kinyang´anyiro," amesema.
Mabadiliko ya katiba tayari yameleta balaa ambapo polisi waliutawanya mkutano wa waandishi habari na viongozi wa upinzani uliokuwa unahusu suala hilo.
Mabadiliko ya katiba yaleta kizazaa na mvutano kati ya serikali na upinzani
Mabadiliko ya hivi karibuni ya katiba yamezusha mjadala kuhusiana na utawala wa Gnassingbe, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005 baada ya kumrithi baba yake, aliyetawala kwa miongo mitatu kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Wakihofia jaribio la kurefushwa utawala wa Gnassingbe, viongozi wa upinzani wanaitaka serikali iyatupilie mbali mabadiliko hayo ya katiba, ambayo yanalipa nguvu bunge kumchagua moja kwa moja rais wa nchi hiyo.
Wanachama 9 wa kundi la upinzani liitwalo Dynamique Monseigneur Kpodzro walikamatwa na polisi kwenye mji mkuu Lome baada ya kuwahutubia watu na kufanya kampeni kwenye soko moja kuelezea kasoro za mageuzi yaliyofanyika.
Hayo yameelezwa na msemaji wa vuguvugu hilo la kisiasa, Thomas Kokou N'soukpoe.
Mwendesha mashtaka wa serikali Talaka Mawama amesema uchanguzi umeanzisha dhidi ya "watu waliokamatwa wakisambaza vipeperushi na kutoa matamshi ya kuchochea vurumai."
Lakini mabadiliko yenyewe ni yapi hasa?
Mnamo mwezi Machi, bunge la Togo lilipitisha sheria ambayo itabadili mfumo wa utawala wa nchi hiyo kutoka ule wenye rais mwenye mamlaka kamili kwenda ule unaolipa bunge nguvu kubwa zaidi.
Maguezi hayo yatalipa bunge uwezo wa kumchagua rais kwa muhula mmoja wa miaka 6. Urais utakuwa wadhifa wa hadhi pekee bila kuwa na madaraka ya kuongoza serikali.
Wabunge watamchagua rais bila kuwepo "mjadala wowote". Hayo ni kulingana na masharti ya katiba mpya. Lakini haiko wazi iwapo rais huyo atakayechaguliwa ataruhusiwa kugombea muhula mwingine.
Mabadiliko hayo pia yataanzisha nafasi ya "kiongozi wa baraza la mawaziri" mfano wa cheo cha waziri mkuu atakayekuwa na madaraka ya kuongoza serikali. Nafasi hiyo pia itajazwa kwa uchaguzi utakaofanywa na bunge.
Mwaka 2019, wabunge wa nchi hiyo waliifanyia mabadiliko katiba kuweka ukomo wa mihula miwili ya rais. Lakini haikufanya kazi kurudi nyuma na hivyo ilimwezesha rais Gnassinbe kugombea chaguzi nyingine mbili.